Elon Musk atangaza kuunda chama kipya Marekani
6 Julai 2025Mgogoro kati ya Rais wa Marekani kutoka chama cha Republican, Donald Trump, na mfadhili wake mkuu wa kampeni Elon Musk umechukua mkondo mpya siku ya Jumamosi, baada ya bilionea huyo wa teknolojia kutangaza kuanzisha chama kipya cha kisiasa. Musk amesema kuwa mswada mpya wa kodi na matumizi uliosainiwa na Trump utaiingiza Marekani kwenye janga la kufilisika.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, siku moja baada ya kuwauliza wafuasi wake kama wanataka chama kipya, Musk alitangaza: "Leo, Chama cha America kimeanzishwa ili kuwarudishia uhuru wenu.” Aliongeza kuwa kura yake ya maoni ilionesha kwa uwiano wa 2 kwa 1, watu wanataka chama kipya — na sasa wanakipata.
Tangazo hilo la Musk limekuja saa chache baada ya Trump kuidhinisha kile alichokiita "mswada mkubwa, mzuri wa kodi” kuwa sheria rasmi, mswada ambao Musk amepinga vikali tangu mwanzo. Kulingana naye, hatua hiyo italiweka taifa kwenye hatari kubwa ya kifedha.
Musk, ambaye ni tajiri namba moja duniani kutokana na mafanikio ya kampuni zake za Tesla na SpaceX, alikuwa ametumia mamilioni ya dola kufadhili kampeni ya Trump na aliongoza Idara ya Ufanisi wa Serikali tangu awamu ya pili ya urais wake, kwa lengo la kupunguza matumizi ya serikali.
Hata hivyo, mara baada ya tangazo hilo la kisiasa kutoka kwa Musk, soko la mitaji lilionyesha dalili za kutoridhika. Kampuni ya uwekezaji ya Azoria Partners imetangaza kuchelewesha kuorodheshwa kwa mfuko wa uwekezaji unaohusiana na Tesla.
Uhusiano na wawekezaji waanza kutetereka
Mkurugenzi Mkuu wa Azoria, James Fishback, alichapisha ujumbe kwenye X akitaka bodi ya Tesla kufafanua malengo ya kisiasa ya Musk. Alisema kuwa hatua hiyo ya kuanzisha chama kipya imewafanya wawekezaji wapoteze imani kuwa Musk angeelekeza nguvu zaidi kwenye kampuni baada ya kujiuzulu serikalini mwezi Mei.
Taarifa za awali ziliashiria kuwa Musk alikuwa tayari kutumia fedha zake binafsi kuwaondoa madarakani wabunge waliounga mkono mswada wa kodi wa Trump. Hali hiyo imeibua taharuki zaidi miongoni mwa wanasiasa wa chama cha Republican.
Trump, kwa upande wake, alitishia kusitisha ruzuku ya mabilioni ya dola inayotolewa na serikali ya shirikisho kwa kampuni za Musk, jambo lililoongeza mvutano kati yao. Wana Republican kadhaa sasa wana wasiwasi kuwa mzozo huu unaweza kuathiri juhudi zao za kudhibiti Bunge katika uchaguzi wa katikati ya muhula mwaka 2026.
Alipoulizwa kwenye X ni jambo gani lilimfanya abadili msimamo kutoka kumpenda Trump hadi kumpinga vikali, Musk alijibu: "Kuongeza nakisi ya bajeti kutoka trilioni 2 wakati wa Biden hadi trilioni 2.5 — hili litafilisi nchi.”
Ikulu ya White House pamoja na Trump hawajatoa tamko rasmi kufuatia tangazo hilo la Musk. Hata hivyo, mvutano huu unaoonekana kuwa baina ya mtu tajiri zaidi duniani na kiongozi mwenye nguvu zaidi duniani, tayari umeathiri bei ya hisa za Tesla.
Hisa za Tesla zilipanda baada ya Trump kuchaguliwa tena Novemba lakini zilifikia kilele mwezi Desemba kabla ya kushuka kwa zaidi ya nusu hadi kufikia dola 315.35 wiki iliyopita.
Licha ya kuwa na uwezo mkubwa kifedha, jaribio la Musk kuvunja mfumo wa vyama viwili uliodumu kwa zaidi ya miaka 160 nchini Marekani litakuwa changamoto kubwa — hasa wakati Trump akiendelea kushikilia zaidi ya asilimia 40 ya umaarufu katika uongozi wake wa pili.