Elon Musk ajiondoa serikalini baada ya kufarakana na Trump
29 Mei 2025Bilionea Elon Musk ametangaza kuondoka katika nafasi yake kama Mfanyakazi Maalum wa Serikali ya Marekani, akisema muda wake uliopangwa umetimia, lakini pia akilalamikia mswada mpya wa matumizi ya serikali uliopitishwa na Rais Donald Trump. Kupitia mtandao wake wa kijamii, X, Musk alimshukuru Trump kwa fursa ya kusaidia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, lakini aliongeza kuwa juhudi za timu yake kupitia Idara ya Ufanisi wa Serikali (DOGE) zimevurugwa na mswada huo.
Musk amesema kuwa mswada huo – uliopitishwa wiki iliyopita na Bunge la Wawakilishi – utaongeza nakisi ya bajeti badala ya kuipunguza, na kwa kiasi kikubwa kudhoofisha juhudi za mageuzi serikalini. Katika mahojiano na televisheni ya CBS News, Musk alisema: "Nilivunjika moyo kuona mswada mkubwa wa matumizi, ambao kimsingi unaongeza nakisi ya bajeti na kuharibu kazi ambayo timu ya DOGE ilikuwa inafanya.”
Musk aliteuliwa na Trump kuongoza juhudi za kubana matumizi serikalini kupitia DOGE, idara iliyoundwa kwa ajili ya kufuta ajira zisizo na tija na kuleta ufanisi wa kiteknolojia serikalini. Tangu kuanzishwa kwake, DOGE iliripotiwa kuwafuta kazi maelfu ya watumishi wa umma, na kufunga idara kadhaa zisizo na matokeo ya moja kwa moja.
Katika hotuba yake ya kuaga, Musk alisema mpango wa DOGE "utaendelea kuimarika kwa muda kama sehemu ya maisha ya kila siku ya serikali,” lakini pia alilalamika kuwa idara hiyo imekuwa "dampo la lawama” kwa matatizo mengi yasiyohusiana nayo moja kwa moja.
Serikali ya Trump ilijitahidi kupunguza mtafaruku uliozuka kwa kusisitiza kuwa mswada uliopitishwa haumaanishi kuwa hakuna nafasi kwa mageuzi kupitia DOGE. Stephen Miller, Naibu Mkuu wa utumishi wa Trump, aliandika kwenye mtandao wa X kwamba "Mswada huo mkubwa hauhusiani moja kwa moja na bajeti ya kila mwaka, na mageuzi ya DOGE yatatekelezwa kupitia mswada tofauti.”
Hata hivyo, kwa wachambuzi wengi, hatua ya Musk ni ishara ya wazi ya mgawanyiko wa nadra kati yake na Rais Trump – mtu aliyemfadhili kwa kiasi kikubwa katika kampeni ya 2024. Inakadiriwa kuwa Musk alitumia zaidi ya dola milioni 250 kuunga mkono kampeni ya Trump kurejea madarakani.
Mashambulizi dhidi ya Tesla na hali ya biashara
Musk pia alifichua kuwa biashara zake ziliathirika pakubwa kutokana na jukumu lake serikalini. Alisema magari ya Tesla yamekuwa yakichomwa moto na waandamanaji waliopinga hatua za kupunguza matumizi ya serikali. "Watu walikuwa wanachoma magari ya Tesla – hilo halikuwa jambo la kiungwana kabisa,” alisema katika mahojiano na Washington Post.
Katika mahojiano hayo yaliyofanyika katika kituo cha uzinduzi wa SpaceX huko Texas, Musk aliongeza kuwa DOGE imekuwa sehemu ya lawama zisizo na msingi. "Ukweli ni kwamba, urasimu wa serikali ya Marekani ni mbaya zaidi kuliko nilivyodhani. Nilijua kuna matatizo, lakini kupambana kuboresha mambo DC ni kama kupanda mlima wa barafu,” alisema.
Licha ya kufutwa kwa ajira nyingi na kufungwa kwa baadhi ya idara, Musk anakiri kuwa hakuweza kufanikisha malengo yote aliyokusudia. Mapungufu hayo yanahusishwa na mtindo wake wa uongozi na kutofahamu kwa undani mienendo ya kisiasa mjini Washington.
Kwa sasa, Musk anasema atajikita zaidi kwenye kampuni zake, hasa baada ya changamoto mfululizo katika SpaceX, ikiwemo mlipuko wa roketi ya Starship wiki hii juu ya Bahari ya Hindi. Aidha, ametangaza kupunguza matumizi yake ya kifedha kwenye siasa, licha ya kuwa mmoja wa wafadhili wakubwa wa kampeni ya Republican.
Vyanzo: Afpe, dpae, Ape