Edinburgh. Waandamanaji kadha wakamatwa katika maandamano ya kupinga utandawazi.
5 Julai 2005Kabla ya mkutano wa kundi la mataifa tajiri yenye viwanda ya G8 hapo Jumatano nchini Scotland, waandamanaji wanaopinga utandawazi duniani wamepambana na polisi mjini Edinburgh.
Polisi wamesema kuwa wamewakamata watu 90.
Polisi pia wamewakamata watu wanne nje ya kituo cha nyambizi za kinuklia za Uingereza katika eneo la Faslane nchini scotland.
Kiasi cha waandamanaji 700 walizuwia milango ya kituo hicho na kuyashutumu mataifa hayo ya G8 kuwa yanahusika na asilimia 90 ya shughuli za biashara ya silaha duniani.
Mkutano huo utakaofanyika katika eneo la Gleneagles nchini Scotland, pia utaangalia kwa kina kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.
Katika mahojiano kabla ya mkutano huo , rais wa Marekani George Bush kwa mara nyingine tena ameukataa mkataba wa hali ya hewa wa Kyoto wa mwaka 1997, akisema kuwa hauna faida kwa uchumi wa Marekani. Badala yake Bwana Bush amesema mkutano huo unapaswa kuanzisha miradi mipya ya pamoja kwa ajili ya teknolojia mpya ya nishati.