Dunia inakabiliwa na chaguo la amani ama vita - Xi
3 Septemba 2025Gwaride la kijeshi lilipita mbele ya umati wa watu zaidi ya 50,000 katika Uwanja wa Tiananmen kuadhimisha miaka 80 tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, ambavyo kwa upande wa China ilikuwa ni ushindi dhidi ya hasimu na mtawala wake, Japan.
Gwaride hilo la Jumatano (Septemba 3) lilijumuisha sio tu wanajeshi wa miguu, bali pia maonesho ya silaha kali za kivita za angani, ardhini na majini.
Helikopta zilizobeba mabango makubwa na ndege za kijeshi ziliruka angani kwa takribani dakika 70, huku njiwa 80,000 wakirushwa kwa ishara ya matumaini ya amani.
Mbali na kuwashukuru washirika wa China katika kile alichokiita "umoja dhidi ya ufashisti uliopata ushindi" kwenye vita hivyo, Rais Xi alisema watu wa China "wamepiga hatua kubwa za maendeleo ya kisasa" na kwamba wapo kwenye upande sahihi wa historia wakati "dunia ikikabiliwa na chaguo baina ya amani au vita."
"Haki, nuru, na maendeleo yatashinda kwa namna yoyote ile dhidi ya uovu na giza. Muda wote, watu wanapaswa kushajiisha maadili ya pamoja kwa wanaadamu wote, kushikilia kwa umakini uadilifu na haki za kilimwengu, na kuachia ukweli uijaze dunia na ulimwengu uangaze kwa nuru." Alisema kiongozi huyo wa China.
Kim, Putin wakutana
Miongoni mwa wageni mashuhuri kwenye maadhimisho hayo walikuwa ni Rais Vladimir Putin na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, ambao baada ya gwaride hilo walikutana kwa mazungumzo ya pande mbili.
Putin alitumia mazungumzo hayo kumshukuru mwenzake kwa mchango mkubwa na "wa kishujaa" wa Pyongyang kwa Moscow inayoendesha vita dhidi ya Ukraine kwa zaidi ya miaka mitatu, akimuita Kim kuwa "ndugu na rafiki wa kuaminika."
Kwa upande wake, Kim Jong Un alisema ni fahari kwa nchi yake kuwasaidia ndugu zao wa Urusi "wakati wowote wanapohitajika" na kwamba ushirikiano wao ni wa muda mrefu na wa kina.
"Tulipigana upande wa ndugu zetu wa Shirikisho la Urusi, na napenda kumshukuru tena Rais Putin kwa kuthamini mchango wetu kwenye mapambano haya. Kama nilivyosema awali, ikiwa kuna lolote ninaloweza kukufanyia wewe (Rais Putin) ama watu wa Urusi, nachukulia hilo kuwa ni wajibu wa udugu ambao niko tayari kuutekeleza kwa moyo mkunjufu." Alisema kiongozi huyo wa Korea Kaskazini.
Korea Kusini, mataifa ya Magharibi na Ukraine yanakisia kuwa Korea Kaskazini ilituma wanajeshi zaidi ya 15,000 kuisaidia Urusi kwenye vita vyake dhidi ya Ukraine.
AFP, Reuters