DRC na M23 waanzisha tena mazungumzo ya amani
7 Mei 2025Mazungumzo hayo yaliyoanza Mei 3, yanafuatia duru ya awali iliyofanyika mwezi Aprili. Afisa mmoja aliye na ufahamu wa karibu na mazungumzo hayo amesema ni mazungumzo chanya, huku pande zote mbili zikiweka matumaini ya kufikia suluhisho.
Vyanzo kutoka kwa waasi wa M23 vimebainisha changamoto zinazoyakumba mazungumzo hayo, ambayo katika duru hii yalikuwa na uwakilishi mdogo kutoka upande wao ikilinganishwa na majadiliano ya mwezi Aprili.
Aidha, walielezea kutoridhishwa kwao kwamba ujumbe wa serikali haukuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi muhimu, jambo linalozuia maendeleo ya mazungumzo.
Hali tete mashariki mwa Kongo
Swala kuu lililozungumziwa na waasi wa M23 ni kushindwa kwa serikali kuchukua hatua madhubuti za kujenga imani, kama vile kuachilia wanachama wa M23 waliokamatwa na Kongo. Hii ni hatua muhimu kwa waasi, kwani wanaona kuwa ni jambo muhimu katika kurejesha imani kwa ajili ya kupata suluhisho la amani.
Wakati mazungumzo huko Doha yanaendelea, hali ya ndani Mashariki mwa Kongo inabaki kuwa tete. Mapigano katika mkoa wa Kivu Kaskazini yamesababisha watu zaidi ya 30,000 kukimbia makwao tangu Ijumaa, kulingana na ofisi ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.
Ghasia zinazozidi zinaonyesha dharura ya mazungumzo ya amani na hitaji la pande zote mbili kupata makubaliano ili kuzuia umwagaji damu unaoendelea.
Mazungumzo ya amani huko Doha yanakuja wakati waasi wa M23 wakiongeza ushawishi wao katika maeneo wanayodhibiti. Katika miji ya Goma na Bukavu, M23 imetangaza kodi mpya kwa biashara za ndani na wafanyabiashara, ikiwemo kodi ya asilimia 15 kwenye uchimbaji wa madini ya coltan, rasilimali muhimu katika eneo hilo.
Hii imeleta changamoto za kiuchumi kwa wakazi na biashara, wengi wao wakiwa wanakutana na ugumu wa kukutana na mahitaji haya mapya.
Mariam Merinde, muuzaji wa ndizi kutoka Goma, alizungumza kuhusu mabadiliko katika maisha yake ya kila siku tangu mgogoro ulipozidi.
"Hali yetu imebadilika tangu tulipokimbia vita. Tulikuwa tunajiendesha vizuri kabla, lakini sasa kila kitu kimebadilika. Sasa tunalipa ada mara mbili za usafirishaji, pamoja na kodi za bidhaa. Hivi ndivyo mambo yalivyobadilika kwa sababu ya hawa waasi na kodi zao nyingi," alisema Marinde.
Macho yote Doha
Jumuiya ya kimataifa, hasa Marekani, imeshiriki katika juhudi za kutafuta makubaliano ya amani. Massad Boulos, mshauri mkuu wa Rais Donald Trump kuhusu Afrika, amesisitiza umuhimu wa makubaliano kamili kati ya Kongo na Rwanda.
Alisema kuwa makubaliano kama hayo hayataleta tu amani bali pia yatafungua uwekezaji mkubwa kutoka Magharibi katika eneo hilo, jambo muhimu kwa ufufuaji wake.
Wakati mazungumzo ya amani yanaendelea, macho yote yameelekezwa Doha, ambako hatma ya mustakabali wa mashariki mwa Kongo inachongwa.
Tumaini ni kwamba majadiliano haya yatafungua njia ya amani ya kudumu na kutoa utulivu unaohitajika kwa ajili ya kuijenga upya mkoa baada ya miaka ya vita vikali.