DRC yaadhimisha miaka 65 ya uhuru katikati mwa mzozo mkubwa
30 Juni 2025Kumbukumbu ambayo inafanyika wakati huu ambapo baadhi ya maeneo ya majimbo ya Kivu kaskazini na Kivu kusini mashariki mwa Kongo yakiwa chini ya waasi waAFC/M23 huku juhudi za kutafuta amani zikiwa zimeendelea huko Marekani na Doha, Nchini Qatar.
Kwa kawaida, bwana Methode Mugwa ni miongoni mwa wakazi wa Bukavu ambaye huandaa tafrija ya kucheza ngoma na marafiki zake kila juni thelathini ili kusherehekea kile wanachokiita "Lipanda”, yaani uhuru wa nchi yake Kongo. Lakini mwaka huu, sherehe hiyo haikuwa kwenye mpango wake.
Mkazi wa Bukavu: Siwezi kusherehekea uhuri wa Kongo kwa sababu tupo vitani
Zaidi bwana Mugwa anasema "Binafsi siwezi kusherehekea uhuru kwa sasa kwa sababu tuko vitani, kwenye migogoro inayojirudia kila siku, nchi imegawanyika na kupigwa na pande zote mbili, nadhani hatuko huru. Suluhu ni kwamba sisi Wakongo tuepuke kudanganywa na nchi za nje zinazotuletea pesa za kuwafanya wenzetu wateseke. Hii ni nchi yetu na lazima tuipende” Aliongeza kwa kusema bwana huyo.
Kwa fursa ya siku hii ya kuadhimisha miaka 65 ya uhuru wa Kongo, Meya wa Washington DC huko nchini Marekani, Muriel Bowser aliitangaza siku hii kuwa "Siku ya raia wamarekani wenye asili ya Kongo"
Wakongo waishio Marekani na mchango wao kwa taifa hilo
Katika taarifa yake, Muriel Bowser amesifu michango ya watu wa asili ya Kongo kwa vikosi vya jeshi, huduma za jamii, elimu, ujasiriamali, huduma za afya, muziki, sanaa na maeneo mengine ambayo amesema yanaboresha sana utamaduni na uchumi wa Marekani hasa katika Wilaya ya Columbia nahata ulimwenguni.
Meya wa Washington pia amesifu muziki wa rumba wa Kongo akisema umepata umaarufu ulimwenguni pote kwa midundo, sauti na maneno yake; hadi kutambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama sehemu ya urithi wa utamaduni usioshikika wa binadamu.
Hatuwa hii imetangazwa siku moja baada ya kusainiwa huko Washington kwa makubaliano ya amani kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda, chini ya uangalizi wa Marekani. Makubaliano hayo yanalenga kumaliza mzozo wa kivita ambao umekuwa ukihatarisha uhusiano kati ya nchi hizi mbili za Afrika kwa takriban miongo mitatu.
Mapendekezo ya kufanyika mkutano kuhusu amani ya Kongo
Licha ya hayo, baadhi ya Wakongo wanasalia na mashaka kwamba makubaliano hayo hayako wazi kabisa kumaliza vita. Zola Mudagi ni mkazi wa Bukavu; anapendekeza kufanyika kwa mkutano mwingine wa kimataifa ili kusuluhisha suala la Kongo mara moja na kwa lote:
Akinukuliwa hapa anasema "Nina huzuni saana moyoni mwangu. Kwa fursa ya leo kila mkongo inabidi afikiri sana. Mikataba hii ni ya kuzubaisha Wakongo. Kwa mzozo wa Kongo, mataifa ya Ulaya na Marekani yanaweza kuwa msingi. Wanajua siri na wanataka kutukengeusha. Suluhu ni kwamba viongozi wa Ulaya lazima waje hapa kwetu na watuambie ni nini hasa wanachotaka hapa kila mara" Alisema Mudagi.
Soma zaidi:Rwanda, DRC zasaini makubaliano ya amani Marekani
Waziri wa Nchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo, Thérèse Kayikwamba Wagner alifafanua kwamba makubaliano yaliyotiwa saini Ijumaa mjini Washington kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda yanaangazia amani mashariki mwa DRC na kwa vyovyote vile sio uuzaji wa rasilimali za madini za Kongo.
Mwenzake wa Rwanda Olivier Nduhungirehe amesisitiza kutokomeza waasi wa Rwanda FDLR wanaojificha mashariki mwa Kongo ili Rwanda iondowe hatua zake za ulinzi Kongo, pia alibainisha kuwa ni mchakato wa Doha utakaowezesha kutatua tatizo kati ya serikali ya Kongo na AFC/M23.
Wakati wakongo wakitarajia kurejea kwa amani, mapigano makali yameripotiwa mwishoni mwa juma kati AFC/M23 na Wazalendo katika vijiji kadhaa vya wilaya ya Walungu jimboni Kivu kusini.
DW, Bukavu