DRC iko katika uelekeo wa kufikia makubaliano ya amani
22 Julai 2025Siku tatu zimepita baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya kanuni huko Doha kati ya serikali ya Kongo na waasi wa AFC/M23 baada ya miezi mitatu ya mazungumzo nchini Qatar. Kanuni hizo zinajumuisha pia kipengele cha "usitishaji wa kudumu wa mapigano".
Itakumbukwa kwamba maelfu ya watu wameuawa nchini Kongo kufuatia mashambulizi ya kundi la waasi wa M23 hasa katika miezi ya Januari na Februari mwaka huu na kupelekea miji muhimu ya Bukavu na Goma kuangukia mikononi mwa waasi hao.
Waziri wa mambo ya ndani wa Kongo Jacquemain Shabani amesema anayo matumaini kwamba awamu hii wako karibu mno kuipata amani nchini Kongo baada ya miongo kadhaa ya ukosefu wa utulivu
"Na leo tumejikuta katika makubaliano ya kanuni na makubaliano ya amani kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Rwanda, na tunasubiri siku ya kusainiwa kwa makubaliano ya amani kati ya muungano wa M23-AFC na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo."amesema Shabani.
Azimio la Doha linajumuisha makubaliano la kurejesha mamlaka kamili ya serikali mashariki mwa Kongo, na makubaliano kwa pande hizo mbili kufungua mazungumzo ya moja kwa moja kuelekea makubaliano ya amani ya kudumu.
Wakongomani wajiandae kwa amani ya kudumu
Waziri wa habari nchini Kongo, Patrick Muyaya, amesema jamii ya Wakongomani inapaswa kujitayarisha kuelekea kufikiwa kwa malengo haya na kwamba rais wa Kongo anayo nia ya dhati ya kufanikisha amani hasa katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
"Rais wa Jamhuri ya Kongo amejitolea kwa dhati kurejesha amani, amani ambayo anatumai itakuwa ya kudumu na ya uhakika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na hasa katika sehemu yake ya mashariki'' amesema Muyaya.
Hata hivyo, licha ya jitihada hizi kutoa matumaini ya kupatikana kwa amani nchini Kongo, bado kuna mashaka yanayotokana na kusambaratika kwa mikataba ya awali ya makubaliano ya kusitisha mapigano mashariki mwa nchi hiyo.
Hapo jana, siku mbili tu baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya kanuni huko Doha kati ya serikali ya Kongo na waasi wa AFC/M23, mapigano yaliripotiwa kuanza tena katika eneo la Kivu Kusini.
Makubaliano hayo yanayolenga kufungua njia ya kusitisha mapigano kwa pande zote mbili, tayari yanaonekana kuwa hatarini.
Rwanda inayotajwa kutoa msaada wa kijeshi kwa M23 inakanusha madai hayo lakini wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema jeshi la Rwanda lilikuwa na jukumu "muhimu" katika mashambulizi ya kundi hilo, ikiwa ni pamoja na operesheni za kivita.