DR Kongo, M23 watoa ahadi ya pamoja kufikia mapatano
24 Aprili 2025Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kundi la waasi la M23 wametoa tamko la pamoja siku ya Jumatano, wakitangaza kuwa wamekubaliana kusitisha mapigano katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Hatua hii mpya imefikiwa baada ya mazungumzo yaliyosimamiwa na Qatar, na ni ya kipekee kwa kuwa makubaliano mengi ya awali ya kusitisha mapigano tangu mwaka 2021 yameshindwa kufanikiwa.
Pande zote mbili zimeahidi kufanya kazi pamoja kufikia mkataba wa amani wa kudumu, na wamesema kuwa watatekeleza usitishaji wa mapigano "muda wote wa mazungumzo hadi yatakapokamilika.” Serikali ya Qatar imekaribisha hatua hii, na kutoa wito kwa pande husika kuendelea na juhudi za kuleta amani ya kweli.
Hatua mpya ya kisiasa katika mgogoro wa DRC
Hii ni mara ya kwanza kwa tamko la kusitisha mapigano kutolewa kwa pamoja na serikali ya DRC na M23. Awali, matamko kama haya yalikuwa ya upande mmoja na mara nyingi yalikiukwa ndani ya muda mfupi. Rais wa DRC Félix Tshisekedi alikuwa amekataa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na M23, akiwashtumu kutumiwa na Rwanda – madai ambayo serikali ya Kigali imekanusha mara kwa mara.
Eneo la mashariki mwa DRC bado ni tete. Licha ya utajiri mkubwa wa madini, eneo hilo limekumbwa na migogoro kwa zaidi ya miaka 30. Tangu M23 walipoanzisha tena vita mwaka 2021, wameteka maeneo muhimu kama vile miji ya Goma na Bukavu. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni saba wamelazimika kuyakimbia makazi yao.
Machungu ya raia: Mapendo na hadithi ya ukombozi
Madhara kwa raia ni makubwa. Katika mtaa wa Panzi, mjini Bukavu, Mapendo M'wa Bushenyula, anawahudumia watoto saba waliokimbia vita, wakiwemo yatima waliopoteza wazazi wao wakati wakikimbia kutoka Nyangezi. Anaishi kwa taabu kubwa, akigawana chakula kidogo na familia nyingi zilizohamishwa.
Soma pia: Serikali ya Kongo na waasi wa M23 wakutana nchini Qatar
"Namuomba Mungu alete amani, watu wasikie, na vita hii iishe. Tunakufa. Watu wawili wa familia yangu waliuawa walipokuwa wakikimbia. Hata pale tunapojificha, risasi zinatufikia. Ndiyo maana tunaomba amani DRC," alisema Mapendo.
Simulizi ya Mapendo inaonyesha namna ambavyo watu wa kawaida wanaumia kutokana na vita hivi. Wamekimbia makazi yao mara kadhaa, na sasa wanakabiliwa na uhaba wa chakula, dawa na makazi. Mashirika ya misaada yanapata ugumu kuwahudumia wahitaji wote.
Matumaini mapya, lakini tahadhari bado ipo
Wakati mazungumzo ya Doha yanatoa matumaini mapya, hali halisi bado ni ya mashaka. Hakuna uthibitisho kutoka vyanzo huru kwamba mapigano yamesimama kabisa. Waasi wa M23, ambao Umoja wa Mataifa unadai wanasaidiwa na wanajeshi kutoka Rwanda, wamewahi kutishia kuendelea hadi mji mkuu wa Kinshasa.
Soma pia: Kongo na waasi wa M23 kuanza mazungumzo ya ana kwa ana
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeanzisha uchunguzi kuhusu madai ya ukatili mkubwa unaofanywa na pande zote mbili, ikiwa ni pamoja na mauaji na ubakaji. Mafanikio au kushindwa kwa usitishaji huu wa mapigano huenda yakawa na athari kubwa kwa hatima ya watu wa mashariki mwa Kongo.