Trump ataka nchi za kiarabu ziwakubali wakimbizi kutoka Gaza
26 Januari 2025Trump aliyetoa kauli hiyo Jumamosi, kulingana na waandishi wa habari amesema kuwa, kila kitu katika eneo hilo kimesambaratishwa na watu wanakufa hivyo angependa kujadiliana na viongozi wa mataifa ya kiarabu na kujenga makazi katika eneo tofauti ili wakaazi hao wa Gaza waishi kwa amani.
Kauli ya Trump imetolewa wakati makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na Hamas, kwa madhumuni ya kuvimaliza kabisa vita hivyo yakiingia wiki ya pili.
Trump ambaye alishafanya mazungumzo na Mfalme Abdullah wa Jordan mapema Jumamosi, ameisifu nchi hiyo kwa kuwakubali wakimbizi wa Kipalestina. Rais huyo wa Marekani aliyeingia madarakani siku kadhaa zilizopita anapanga pia kufanya mazungumzo na Rais wa Misri Abdel Fattah El Sissi leo Jumapili.
Hayo yanajiri wakati ambapo Trumpameliamuru jeshi lake kuruhusu kuyapeleka mabomu 2,000 Israel, yaliyozuiwa awali na mtangulizi wake, Joe Biden. Biden alizuia kupelekwa kwa silaha hizo Israel kwa kuhofia madhara kwa raia hasa wakaazi wa Rafah katika Ukanda wa Gaza wakati wa vita vya Israel katika eneo hilo.