DOHA: Kitisho cha mashambulio zaidi Uingereza
2 Septemba 2005
Mshambuliaji mmojawapo kati ya wale waliojitoa muhanga katika mashambulio ya London,ameonyeshwa kwenye kanda ya video.Mohamed Siddique Khan katika kanda hiyo amehusisha mashambulio ya bomu mjini London na msimamo wa Uingereza kuunga mkono vita vya Iraq.Katika kanda hiyo ya video iliyo onyeshwa kwenye televisheni ya kiarabu Al Jazeera,Mohammad Siddique Khan katika risala aliyotoa kabla ya kifo chake ameonya kuwa kutafanywa mashambulio zaidi.Stesheni ya Al Jazeera ilitangaza pia matamshi ya makamu wa Osama Bin Laden,Ayman al-Zawahri.Katika kanda ya video ya mwezi uliopita,inayosemekana kuwa ni ya mtandao wa Al Qaeda,Waingereza wameonywa kuhusu mashambulio zaidi na kuambiwa kuwa siasa za waziri mkuu wa Uingereza,Tony Blair zitasababisha maafa zaidi kwa Waingereza.Watu 52 waliuawa katika mashambulio ya mwezi Julai mjini London.Katika mashambulio hayo basi moja na treni tatu zinazosafiri chini ya ardhi ziliripuliwa kwa mabomu na washambuliaji waliojitoa muhanga.