Dini ya Kiislam kujihusisha na mipango ya kuhifadhi maji, Mashariki ya Kati.
24 Mei 2005Mipango iko mbioni huko Qartar kujenga vipimo vya maji katika misikiti kwa lengo la kuweka kumbu kumbu ya matumizi ya maji. Inaripotiwa kuwa eneo la Mashariki ya Kati, ni miongoni mwa maeneo yanayotumia maji kwa kiwango cha hali ya juu duniani.
Hatua ya kuhusisha dini ya kiislamu na zoezi la kudhibiti matumizi ya maji imearifiwa kuwa si mpya, kwani dini ya kiislamu imekuwa ikihimiza matumizi mazuri ya maji pamoja na mali asili nyingine . Lakini kampuni ya maji na umeme nchini Qartar imeanzisha zoezi hilo kwa lengo la kuepusha matumizi yasiyo ya lazima ya maji, na pia kuweza kuyahifadhi vizuri.
Vipimo vya namna hiyo vya maji vinatarajiwa kujengwa kwenye majengo yote ya serikali. Hii ni kwa ajili ya kuwahimiza wananchi juu ya umuhimu wa kutunza maji, kwani maji ni mali asili muhimu nchini Qartar, amesema Khalid Al Mansouri , mkurugenzi wa mtandao wa usambazaji maji nchini humo.
Misikiti yote nchini Qartar inayo mabomba makubwa makubwa kwa ajili ya shughuli maalum ya kutawadha kabla ya sala. Kawaida , misikiti yote hupata misaada ya mashine za kupoza maji ya kunywa kutoka kwa waumini wafadhili.
Hata hivyo, matumizi ya maji na hata idadi ya watu wanaoingia misikitini kipindi cha sala haijulikani. Watu wengine jirani na misikiti hiyo pia hutumia kiasi kikubwa cha maji kwa ajili ya matumizi yao binafsi, kama vile kufua na kuosha magari yao.
Matumizi ya maji katika eneo la Mashariki ya Kati ni ya hali ya juu katika nchi zote za umoja wa falme za kiarabu kiasi cha kuzidi lita 378.5 kwa mtu mmoja kila siku, ikilinganishwa na kiwango cha kimataifa kinachohimiza matumizi ya maji galoni 189 hadi 265 kwa siku. Kiwango cha matumizi ya maji kimepanda kutoka asilimia 8 hadi 10 kwa mwaka.
Utafiti uliofanywa na shirikisho la kuhifadhi mazingira unabainisha kwamba takriban galoni 630 zilitumiwa kila siku mwaka 2000 ambapo matumizi hayo yanatarajiwa kupanda hadi kufikia lita bilioni 2.3 mwaka huu. Kiwango hicho kitapanda na kufikia bilioni 4.7 ifikapo mwaka wa 2010. Kwa mujibu wa utafiti huo, cha kushangaza ni kwamba matumizi ya maji yanazidi kuongezeka wakati ambapo vina vya maji vinapungua katika vyanzo vyake.
Maji yamekuwa yakipungua kwa kiasi cha mita moja kila mwaka kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita. Mtafiti wa masuala ya matumizi ya maji katika kampuni ya maji huko Dubai, Bwana Essam Al Muhairi , amesema ongezeko la matumizi ya maji linazidi kutokana na sababu tatu zinazopelekea mahitaji ya matumizi hayo hususan kasi ya ongezeko la watu, kukua kwa vivanda na kilimo na pia mabadiliko ya hali ya hewa.
Nchini Dubai pekee, moja ya falme za kiarabu, usambazaji wa huduma za maji ni kubik lita laki mbili na kumi kwa siku, na inakisiwa kwamba kiasi hicho kitapanda kwa zaidi ya mara tatu na kufikia kubik lita laki sita na sitini, ifikapo mwaka wa 2020.
Nchi sita zinazounda umoja wa falme za kiarabu, kwa pamoja zimetumia zaidi ya dola za kimarekani bilioni 40 kwa ajili ya kujenga vituo na visima vikubwa vya maji chini ya ardhi katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.