Denmark na Ujerumani zataka Ulaya iliyo thabiti
28 Januari 2025Friedriksen amesema "Tunakabiliwa na sintofahamu iliyo dhahiri, ukweli unaohitaji Umoja wa Ulaya kushikamana zaidi. Tunaona mashambulizi mchanganyiko ya Urusi. mashambulizi barani Ulaya, katika bahari ya Baltiki, vita vya uchokozi barani Ulaya, na kwa bahati mbaya... sasa kuna ushirikiano kati ya Urusi, Iran na Korea Kaskazini."
Friedriksen amesema hayo hii leo baada ya kukutana na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Berlin na kuzungumzia masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na vita vya Urusi nchini Ukraine.
Friedriksen aliweka kituo mjini Berlin katika sehemu ya ziara yake kwenye miji mikuu ya mataifa makubwa ya Ulaya, katikati ya kitisho dhidi ya bara hilo ambacho mwenyewe amekiita "sintofahamu dhahiri". Kiongozi huyo pia atatembelea Paris na Brussels.
Soma pia:Trump akosolewa kwa kuashiria kuzitwaa Greenland, Canada
Lakini pia ni ziara anayoifanya wakati Rais wa Marekani Donald Trump akiwa tayari amesema hataondoa uwezekano wa kutumia jeshi kuidhibiti Greenland, kwa kile alichosema "usalama wa kimataifa". Greenland ni nchi iliyopo chini ya utawala wa Kifalme wa Denmark.
Siku ya Jumatatu, serikali ya Denmark ilitangaza karibu dola bilioni mbili, ambazo ni sehemu ya makubaliano na Visiwa vya Faeroe ya kuimarisha uwepo wa jeshi kote nchini Greenland.
Kansela Scholz alaani kauli za "udhibiti wa maeneo"
Kansela Scholz kwa upande wake amenukuliwa akisema "Hizi ni nyakati ngumu" na zinahitaji Ulaya na NATO zenye nguvu.
"Pamoja na operesheni ya NATO, tutaboresha ulinzi kwenye Bahari ya Baltiki na miundombinu muhimu kwenye bahari. Ni wazi kwamba NATO inabakia kuwa mdhamini wa usalama wetu, ndiyo maana washirika wengi wameongeza matumizi ya ulinzi kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni, ndio maana Finland na Sweden wamejiunga na NATO."
Scholz kwa mara nyingine amelaani vikali unyakuzi wa maeneo, bila ya kujali ni nani hasa anafanya vitendo hivyo. Scholz amesema "mipaka haitakiwi kuhamishwa kinguvu" na kumalizia kwa kusema, limfikie yoyote anayehusika. Amesema ni lazima kila mmoja kuheshimu kanuni za kimataifa zinazohusiana na mipaka.
Lakini, matamshi yake yalikuwa dhahiri kwamba yalimlenga Trump ambaye amenukuliwa mara kadhaa akitoa matamshi yanayoashiria kuchukua baadhi ya maeneo, ambayo ni pamoja na Mfereji wa Panama huku akionyesha kuitamani Canada kujiunga na Marekani.
Mjini Paris, Friedriksen atakutana na Rais Emmanuel Macron, kabla ya kwenda Brussels ambako atazungumza na Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte.