Dada wa Kim Jong Un aishambulia serikali ya Korea Kusini
20 Agosti 2025Ameishambulia nchi hiyo jirani kwa hatua yake ya kufanya luteka ya kijeshi na Marekani huku ikijaribu kuinyooshea mkono wa urafiki Korea Kaskazini.
Kupitia taarifa yake iliyochapshwa na shirika la habari la Korea Kaskazini, Kim Yo Jong, amesema utawala wa Korea Kusini unatekeleza "sera za kuicheza shere" serikali mjini Pyongyang kupitia matamshi ya kirafiki wakati inashirikiana kwa karibu na Marekani, iliyo hasimu wa Korea Kaskazini.
Matamshi yake yanafuatia ahadi iliyotolewa hivi karibuni na rais mpya wa Korea Kusini, Lee Jae Myung aliyesema anataka kurekebisha mahusiano kati ya Korea Mbili na kupunguza mivutano ya miaka mingi.
Hata hivyo Bibi Yong amesema mazoezi ya kijeshi yaliyoanza Jumatatu kati ya Korea Kusini na Marekani ni uthibitisho wa tabia ya kuwa sura mbili ya viongozi mjini Seoul.