China yaweka ´kigingi´ matakwa ya kibiashara ya Marekani
4 Agosti 2025Baada ya siku mbili za mazungumzo jijini Stockholm, pande zote zilionyesha nia ya kusuluhisha tofauti zao lakini msimamo wa Washington wa kuitaka China kusitisha biashara hiyo ya nishati bado ni kikwazo kikuu.
Msimamo wa China wa kukataa shinikizo hilo unaangazia jinsi Beijing inavyolipa kipaumbele suala la nishati kama sehemu ya sera yake ya kigeni na usalama wa taifa.
Katika ujumbe uliochapishwa kwenye mtandao wa X, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilisisitiza kuwa "China daima itahakikisha usalama wa nishati yake kwa njia zinazolinda maslahi ya taifa,” na kuongeza kuwa "vitisho na mashinikizo haviwezi kuleta mafanikio.”
Kauli hiyo imeonesha wazi kuwa Beijing haitakubali kushinikizwa katika masuala ya nishati, na inalitazama suala hilo kama msingi wa uhuru wake wa kidiplomasia na wa kiuchumi.
Mtazamo huu wa China umekaririwa pia na Msemaji wa wizara ya mambo ya Nje ya China Guo Jiankun ambaye amesema;
"Msimamo wa China dhidi ya ushuru wa kiholela wa forodha umekuwa wa wazi na thabiti. Hakuna mshindi katika vita ya ushuru au vita ya kibiashara. Kulinda masoko kwa misingi ya kitaifa kunadhuru pande zote zinazohusika."
Washington yatishia kutumia ´rungu´la vikwazo dhidi ya Beijing
Marekani imetishia kuiwekea China ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa zake kama njia ya kuilazimisha ikubali masharti ya kimataifa kuhusu ununuzi wa mafuta.
Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent, amekiri kuwa Wachina ni "wajanja” katika majadiliano, lakini ameongeza kuwa suala la mafuta halijavuruga mchakato mzima wa mazungumzo.
Hata hivyo, wachambuzi wanatahadharisha kuwa utekelezaji wa vitisho hivyo unaweza kufuta mafanikio yote ya kidiplomasia na kuharibu uwezekano wa makubaliano kati ya Rais Trump na Rais Xi Jinping.
China kwa sasa ndiyo mnunuzi mkuu wa mafuta kutoka Iran — ikiwa inachukua kati ya asilimia 80 hadi 90 ya mauzo ya mafuta ya nchi hiyo, zaidi ya mapipa milioni moja kwa siku.
Kwa upande wa Urusi, China ilinunua zaidi ya mapipa milioni 1.3 kwa siku mwezi Aprili pekee, kwa mujibu wa taasisi ya utafiti ya KSE nchini Ukraine.
Biashara hii ya mafuta si tu kwamba inaimarisha uchumi wa China, bali pia inazipatia Iran na Urusi mapato muhimu katika kipindi ambacho zimewekewa vikwazo na Marekani.
Wataalamu wanasema China inaamini kuwa mafuta kutoka Iran na Urusi ni nguzo muhimu kwa usalama wake wa kiuchumi na kisiasa.
Wanasiasa wa Marekani waanzisha jitihada za kuongeza shinikizo
Kutoitii Marekani kunatazamwa kama njia ya kuonyesha mshikamano na Moscow huku ikiendelea kupunguza utegemezi wake kwa vyanzo vya nishati kutoka nchi rafiki za Marekani.
Aidha, Beijing inaona sera za Marekani kuhusu Urusi na Iran kuwa zenye mgongano na zisizo na msimamo wa pamoja, hali inayoiwezesha kujadiliana kwa ujasiri zaidi.
Kwa upande mwingine, Marekani inazidi kuimarisha shinikizo kwa njia ya vikwazo. Seneta Lindsey Graham ameanzisha mswada wa sheria unaoruhusu ushuru wa hadi asilimia 500 kwa nchi "zinazojua” zinanunua mafuta kutoka Urusi, hatua inayolenga kukomesha ufadhili wa vita ya Putin dhidi ya Ukraine.
Mswada huo umeungwa mkono na wabunge kutoka vyama vyote viwili vikuu vya kisiasa nchini Marekani.
India, kama China, ni mnunuzi mkubwa wa mafuta ya Urusi. Rais Trump ametangaza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa kutoka India, akilalamikia kwamba hatua hiyo ya manunuzi ya mafuta inaifanya India kuwa miongoni mwa wafadhili wa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.
Ikulu ya Marekani imesisitiza kuwa si haki kwa mataifa kama India au China kunufaika kiuchumi huku yakiepuka matokeo ya kisiasa ya migogoro ya kimataifa.
Ingawa pande zote mbili — Marekani na China — zimeonyesha nia ya kufikia makubaliano ya biashara, mvutano kuhusu mafuta umebainisha kuwa si kila jambo linaweza kujadiliwa mezani. Kwa China, nishati si suala la kiuchumi tu — ni suala la msingi la usalama wa taifa.