China yawaalika Iran na Urusi kwenye mkutano wa SCO
26 Juni 2025Mkutano huu unafanyika wakati dunia ikishuhudia mivutano ya kijeshi Mashariki ya Kati na Ulaya, huku nchi wanachama wa NATO zikiahidi kuongeza bajeti zao za ulinzi baada ya kikao cha kilele huko The Hague.
Jumuiya ya SCO yenye wanachama 10 ikiongozwa na China na Urusi, inajitambulisha kama jukwaa mbadala kwa miungano ya kijeshi inayoongozwa na Magharibi.
Mkutano huu wa Qingdao umeangazia juhudi za kukuza ushirikiano wa kijeshi, kisayansi, kiusalama na kiuchumi baina ya wanachama wake, sambamba na kusisitiza umuhimu wa utulivu katika Mashariki ya Katikufuatia makubaliano ya kusitisha vita vilivyodumu kwa takribani wiki mbili kati ya Iran na Israel.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri wa Ulinzi wa China Dong Jun alionya kuhusu kuongezeka kwa machafuko na hali ya kutoaminiana duniani. Alikosoa vikali sera za upande mmoja na ulinzi wa kimaslahi, akiziita tishio kwa utaratibu wa kimataifa. "Vitendo vya kiubabe, vya kidomino na vya kijeuri vinadhoofisha sana utaratibu wa kimataifa,” alisema Dong, akizitaka nchi wanachama kuchukua hatua madhubuti zaidi kulinda mazingira ya maendeleo ya amani.
Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Andrei Belousov, alikubaliana na msimamo huo wa China na akaongeza kuwa hali ya kisiasa na kijeshi duniani imezidi kuzorota. Alilaumu mataifa ya Magharibi kwa kupeleka silaha na mamluki nchini Ukraine, akisema hatua hizo zinachochea machafuko barani Ulaya.
Vikosi vya Urusi vinaendesha mashambulizi kwa mafanikio. Utawala wa Kyiv unaelewa kuwa kushindwa kwake hakuepukiki, hivyo unawekeza katika mashambulizi ya kigaidi. Juhudi za kurefusha vita kwa kuiuzia Ukraine silaha na kupeleka mamluki zinaongeza tishio la kuyumba, hata ndani ya Ulaya yenyewe. Wakati huo huo, Urusi imekuwa ikisisitiza mara kwa mara utayari wake wa kutafuta suluhisho la mzozo huu.
Mkutano huu unafanyika wakati nyeti kwa uhusiano wa China na washirika wake wakuu, Urusi na Iran. Ingawa Beijing inadai kutoegemea upande wowote katika vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, wachambuzi wanasema imeendelea kutoa msaada wa kiuchumi na kidiplomasia kwa Moscow. Wakati wa mzozo wa hivi karibuni kati ya Iran na Israel, China ilitoa tu misimamo ya maneno, ikiepuka kuchukua hatua zinazoweza kuathiri uhusiano wake na Marekani
Wito watolewa kwa wanachama wa SCO kushirikiana zaidi
Wachambuzi wanaamini kuwa China haina nia ya kuipatia Iran msaada wa kijeshi moja kwa moja. "Msaada wa maneno ndiyo kiwango cha juu ambacho Beijing itaenda,” alisema James Char kutoka Singapore. Aidha, baadhi wanaamini Iran inaweza kujaribu kushinikiza kupewa silaha, lakini Beijing haitakubali kwa hofu ya kuchochea uhasama kutoka Israel au Marekani.
Waziri wa Ulinzi wa India, Rajnath Singh, alitoa wito kwa wanachama wa SCO kushirikiana zaidi katika kukabiliana na changamoto za kimataifa. Alieleza kuwa kasi ya utandawazi imepungua, na akaonya kuwa ni muhimu kwa mataifa kuungana na kurekebisha mikakati yao ya usalama na ushirikiano wa kimataifa.
Huku SCO ikionekana kutaka kupinga misimamo ya kambi ya Magharibi, tahadhari ya China — hasa Mashariki ya Kati — inaonesha mipaka ya ushawishi wake wa kimataifa mbele ya migongano tata ya kimataifa na miungano iliyoegemea kambi pinzani.