China yaikosoa Marekani kwa 'uonevu' ikitafuta ushawishi LAC
13 Mei 2025China imetangaza kuimarisha ushirikiano wake wa kimkakati na mataifa ya Amerika ya Kusini na Karibiani (LAC) kupitia ahadi ya maendeleo na ukosoaji mkali wa kile ilichokiita "uonevu wa kimataifa", wakati Rais Xi Jinping alipowahutubia viongozi wa kikanda katika mkutano wa Jukwaa la China-CELAC uliofanyika mjini Beijing.
Katika mkutano huo wa kilele, Rais Xi alitangaza mkopo wa dola bilioni 9.2 kwa nchi za LAC kwa ajili ya miradi ya maendeleo, huku mkopo huo ukitolewa katika sarafu ya China – Yuan – hatua inayolenga kupanua ushawishi wa kifedha wa Beijing na kupunguza utegemezi wa dola ya Marekani.
Akiwahutubia viongozi hao akiwemo Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva, Rais wa Colombia Gustavo Petro na Rais wa Chile Gabriel Boric, Xi alitumia jukwaa hilo kuonyesha hadharani kuchukizwa kwake na sera za Marekani – bila kuitaja moja kwa moja – akisema kuwa "unyanyasaji na ubabe vitaishia kwenye kujitenga.” Alisisitiza kuwa "hakuna washindi katika vita vya ushuru au biashara” na kwamba "umoja na ushirikiano ndiyo njia pekee ya kulinda amani na utulivu duniani.”
Katika sauti yake ya moja kwa moja, Xi alisema: "China na nchi za Amerika ya Kusini na Karibiani ni wanachama muhimu wa ulimwengu wa Kusini. Uhuru na kujitegemea ni urithi wetu wa fahari. Maendeleo na uhuishaji ni haki yetu ya msingi. Na haki na usawa ni azma yetu ya pamoja. China iko tayari kushirikiana kwa dhati katika mipango mitano ya pamoja kwa ajili ya maendeleo ya pamoja."
Ushirikiano wazidi kuimarika
China imeendelea kuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara kwa nchi kama Brazil, Chile na Peru – ikiipiku Marekani katika eneo hilo. Takriban theluthi mbili ya mataifa ya LAC yamejiunga na mpango wa China wa miundombinu wa Belt and Road Initiative (BRI), huku Colombia ikitarajiwa kusaini makubaliano wakati wa ziara ya Rais Petro mjini Beijing.
Soma pia: IMF yashusha makaridio ya ukuaji wa uchumi wa dunia
Katika mkutano huo, Xi pia alitangaza hatua mpya za urahisishaji wa usafiri kwa baadhi ya nchi za LAC kwa kuondoa mahitaji ya visa – ingawa hakutaja ni nchi zipi. Aidha, aliahidi ushirikiano zaidi katika nyanja za nishati safi, miundombinu, kupambana na ugaidi na uhalifu wa kimataifa, pamoja na kubadilishana masomo na mafunzo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, aliendelea kuikosoa Marekani, akisema kuna "mamlaka kubwa inayotumia ushuru kama silaha ya kuonea nchi nyingine,” na kuzihimiza nchi za LAC kuungana na China kulinda haki zao. Alisema mkutano huo ulikuwa "sukari ya diplomasia,” ukifungua soko kubwa la watu bilioni mbili linaloweza kukuza uchumi kwa pande zote mbili.
Majibu kwa siasa za Trump
Mkutano huo umejiri wakati ambapo Rais wa Marekani Donald Trump anazidi kushinikiza nchi za Amerika ya Kusini kuchagua upande kati ya Washington na Beijing. Ingawa Marekani na China zilitangaza kusitisha ushuru mpya kwa siku 90, mvutano kuhusu biashara na masuala ya madawa ya kulevya kama fentanyl bado unaendelea.
China kupitia wizara yake ya mambo ya nje, ilitaka Marekani "kuacha kueneza lawama” kuhusu mgogoro wa opioidi na badala yake kushughulikia chanzo halisi cha tatizo hilo.
Katika hali inayoonyesha mabadiliko ya mwelekeo wa kidiplomasia, China na Brazil pia walitoa taarifa ya pamoja ya kuunga mkono pendekezo la Rais Vladimir Putin la kuanza mazungumzo ya moja kwa moja ya amani na Ukraine — wakisisitiza kuwa ni njia pekee ya kumaliza mzozo huo.
Kwa ujumla, mkutano wa CELAC mjini Beijing umeonesha dhamira ya China kujitanua zaidi katika Amerika ya Kusini, huku ikitumia sera za maendeleo na diplomasia ya ushirikiano kama mbinu za kushawishi, sambamba na kuendeleza ushindani wake wa kimkakati dhidi ya Marekani.