China yafanya luteka za kijeshi kuzunguka Taiwan
1 Aprili 2025Matangazo
China imefanya luteka kubwa za kijeshi Jumanne kukizunguka kisiwa cha Taiwan kuwa kama onyo kali kwa kisiwa hicho kinachojitawala kidemokrasia dhidi ya kujitenga.
Shi Yi, msemaji wa Kamandi ya Mashariki ya jeshi la Ukombozi la umma wa China ameyaita mazoezi hayo ya kijeshi kama onyo kali na kizuizi cha nguvu dhidi ya uhuru wa Taiwan.
Kikosi cha China cha ulinzi wa pwani kimeziita luteka hizo kama doria ya utekelezaji wa sheria kuizunguka Taiwan.
Wizara ya ulinzi ya Taiwan imefuatilia meli 19 za jeshi la majini la China ikiwemo meli ya kubebea ndege za kivita ya Shandong, iliyoingia katika eneo la ulinzi la Taiwan.
Katika hatua ya kujibu, Taiwan imepeleka meli za kivita na kuamilisha mifumo yake ya ulinzi dhidi ya makombora.