China yaendelea na luteka za kijeshi kuizunguka Taiwan
2 Aprili 2025Jeshi la China limesema limefanya mazoezi ya kuzilenga bandari muhimu na vituo vya nishati wakati wa mazoezi ya kutumia risasi za moto kama sehemu ya luteka zinazoilenga Taiwan, kisiwa ambacho China inasema ni himaya yake. Mazoezi hayo ya kushangaza yamekosolewa na Marekani kama mbinu ya vitisho na yanafanyika baada ya rais wa Taiwan Lai Ching-te kuiita China kuwa ni nguvu ya kigeni ya uadui.
Jeshi la China limesema hivi leo kwamba linaendelea na mazoezi ya kijeshi katika maeneo ya bahari yanayokizunguka kisiwa cha Taiwan. Msemaji wa kamandi ya mashariki ya jeshi la China, Shi Yi, amesema katika siku ya pili ya luteka hizo, kwamba vikosi vilikuwa vikifanya mazoezi katika eneo la kati na kusini mwa mlango bahari wa Taiwan. Yi amesema mazoezi hayo yanajumuisha mashambulizi yanayoyalenga maeneo maalumu ya kuigwa yanayonuiwa kushambuliwa.
China yafanya mazoezi mengine ya kijeshi Taiwan
Mazoezi hayo yamepewa jina Strait Thunder - 2025A, jina linalopendekeza kwamba kuna mengine yatakayofuata baadaye mwaka huu. Mwaka uliopita China ilifanya mazoezi makubwa ya kijeshi mara mbili kukizunguka kisiwa cha Taiwan mnamo mwezi Mei na Oktoba, yaliyopewa majina ya Joint Sword-2024A na Joinst Sword-2024B.
Mazoezi hayo ya pamoja yaliyolijumuisha jeshi la nchi kavu, jeshi la wanamaji, jeshi la anga na kitengo cha makombora yalianza jana Jumanne. Kufikia jana mchana wizara ya ulinzi ya Taiwan ilikuwa imezitambua ndege za kivita za China, meli 21 za vita, ikiwemo manowari moja na meli nne za walinzi wa pwani nje ya visiwa vyake.
Taiwan yafuatilia kwa karibu mazoezi ya kijeshi ya China
Wizara ya ulinzi ya Taiwan imesema imekuwa ikifuatilia mienendo ya mali za kijeshi za jeshi la China tangu Jumamosi. Pamoja na mazoezi ya kawaida ya kijeshi, ndege za kivita za China huruka karibu kila siku katika eneo la ulinzi la Taiwan, jambo linalolilazimu jeshi la anga la Taiwan kuchukua hatua ya kujibu.
China imetahadharisha leo kupitia msemaji wake wa wizara ya mambo ya nje, Guo Jiakun kwamba adhabu kwa Taiwan itaendelea hadi pale viongozi wake watakapowachana na juhudi za kushinikiza kile ambacho serikali ya mjini Beijing inasema ni uhuru kutoka kwa China bara.
"Alimradi uchochezi wa uhuru wa Taiwan unaendelea, adhabu dhidi ya uhuru haitakoma. Hatutamruhusu mtu yeyote, nguvu yoyote, kwa njia yoyote kuitenganisha Taiwan kutoka kwa China. Tutachukua hatua zote zinazohitajika ili kuulinda kwa uthabiti uhuru wa taifa na uadilifu wa eneo letu."
Wizara ya mambo ya nje ya China imewahimiza viongozi wenye nyadhifa muhimu nchini Ufilipino wasitoe kauli zisizo na msingi kuhusu suala la Taiwan, ikitahadharisha kwamba wale wanaocheza na moto, utawachoma wenyewe.
China yafanya luteka za kijeshi kuzunguka Taiwan
Kauli ya msemaji wa wizara hiyo Guo Jiakun katika mkutano wa mara kwa mara na waandishi habari imekuja kama jawabu kwa mkuu wa majeshi ya Ufilipino Romeo Brawner akiwaambia wanajeshi waanze kujiandaa na kupanga kuchukua hatua ikiwa kutatokea uvamizi dhidi ya Taiwan.
Wizara ya ulinzi ya Taiwan imesema hivi leo kwamba haijabaini mazoezi ya China ya kutumia risasi za moto, ingawa imesema China ilifanya hivyo nje ya pwani ya mkoa wa mashariki wa Zhejiang.