China ina jibu gani kuepuka vita vya ushuru na Marekani?
9 Aprili 2025Beijing, inayohisi kubanwa na hatua kali za Marekani za kutoza ushuru bidhaa za China na nchi yoyote ambayo inanunua au kutengeneza vitu kwa kutumia vipuri vya China, inajiandaa kwa vita vya kiuchumi.
Washington wiki iliyopita iliweka ushuru wa forodha wa 10% kwa bidhaa kutoka karibu dunia nzima, na ushuru wa juu zaidi kwa nchi kama vile Vietnam, ambakoo viwanda vya China vimekuwa vikihamishia shughuli za uzalishaji. Hii ilisababisha hatua ya kulipiza kutoka kwa China, ikifuatiwa na vitisho vipya kutoka kwa Rais wa Merikani Donald Trump.
Mshauri mmoja wa sera za China anasema atakayesalimu amri wa kwanza atakuwa muathiriwa. Mshauri huyo ambaye hajataka kutajwa jina kutokana na unyeti wa mada hii anasema ni suala la muda tu kuona atakayevumilia kwa muda mrefu zaidi.
China hata hivyo haina chaguzi nzuri. Itatafuta masoko mengine barani Asia, Ulaya na kwingineko duniani, lakini hii inaweza isiwe njia bora ya kujikwamua.
Nchi nyingine zina masoko madogo zaidi kuliko Marekani, na uchumi wa mataifa mengine unaathirika kutokana na ushuru huo. Nchi nyingi pia zinahofia kuruhusu bidhaa za bei nafuu zaidi kutoka China.
Kuishusha thamani ya sarafu itakuwa njia rahisi zaidi ya kupunguza athari za ushuru nchini China lakini hiyo inaweza kusababisha uhamishaji wa mtaji kwenda nchi za kigeni, wakati pia ikiwatenga washirika wa kibiashara ambao China inaweza kujaribu kushirikiana nao.
Ruzuku zaidi, punguzo la kodi ya mauzo ya nje au aina nyingine za kichocheo zinaweza kutumika, lakini hii pia inaweza kuhatarisha kuzidisha uwezo wa kiviwanda na kuchochea shinikizo zaidi la kupungua kwa bei za bidhaa.
Wachambuzi kwa miaka mingi wamekuwa wakitetea sera ambazo zinaweza kuongeza mahitaji ya ndani. Lakini licha ya matamko ya Beijing, sio mengi yaliyofanywa kuongeza matumizi, ikizingatiwa kwamba mabadiliko ya kisera ambayo yangehitajika yanaweza kuharibu sekta ya utengenezaji katika kipindi cha muda mfupi.
Kujibu kwa kutangaza ushuru wake na kudhibiti mauzo ya nje kunaweza kusiwe na ufanisi sana, ikizingatiwa China inapeleka Marekani karibu mara tatu ya bidhaa kuliko biadhaa inazoingiza za karibu dola bilioni 160. Lakini linaweza kuwa chaguo pekee ikiwa Beijing inaamini kuwa lina kiwango kikubwa zaidi cha maumivu kuliko ilicho nacho Washington.
Arthur Kroeber, mkuu wa utafiti katika kampuni ya huduma za fedha ya Gavekal iliyoko Hong Kong anasema China haiwezi kusababisha maumivu mengi kwa Marekani kama inavyopokea, kwa kuwa inaendesha biashara kubwa, na ando na madini adimu, bado inaweza kupata hasara zaidi kutokana na udhibiti wa mauzo ya nje.
Pamoja na Washington na Beijing kujaribu kumuumiza kila mmoja na ulimwengu wote ukionekana kujikuta katikati ya vita vyao vya kibiashara, ni ngumu kufikiria jinsi mpango mkubwa wa kupunguza mvutano huo unavyoweza kuwa.