Chelsea yatinga fainali ya Kombe la Dunia kwa vilabu
9 Julai 2025Klabu ya soka ya Chelsea ya nchini Uingereza imeweka rekodi mpya ya kuwa klabu ya kwanza duniani kutinga katika fainali ya michuano ya Kombe la Dunia linalosimamiwa na Shirikisho la Soka Duniani FIFA baada ya kuichakaza timu ya Fluminense ya nchini Brazil kwa mabao mawili kwa nunge katika mchezo wa nusu fainali nchini Marekani.
Mchezaji wa Chelsea Joao Pedro aliyesajiliwa wiki iliyopita tu na klabu hiyo ameyatupia kambani magoli yote mawili na kuivusha timu hiyo kwenda fainali. Pedro ambaye ni raia wa Brazil aliwahi pia kuichezea timu ya Fluminense ambayo ameisaidia Chelsea kuitupa nje ya michuano hiyo.
Chelsea itamenyana na Real Madrid au Paris St Germain, katika mchezo wa fainali siku ya Jumapili, Madrid na PSG zitakutana hii leo kwa mchezo wa nusu fainali ya pili.