Chanjo kutoka Afrika: Nyota njema yachomoza
22 Agosti 2025Janga la COVID-19 limechochea harakati mpya barani Afrika za kujitegemea katika uzalishaji wa dawa na chanjo ili kupunguza utegemezi mkubwa wa uagizaji kutoka nje. Upungufu na usambazaji usio sawa wa chanjo wakati wa mlipuko huo uliweka wazi udhaifu wa mifumo ya afya barani humo na kuamsha dhamira ya kuwekeza zaidi katika sekta ya afya na teknolojia za tiba.
Mlipuko wa janga la COVID-19 mwaka 2020 ulidhihirisha kwa namna ya kutisha, utegemezi wa Afrika kwa chanjo kutoka nje. Ingawa chanjo za COVID-19 zilichukuliwa kama hatua muhimu ya kudhibiti maambukizi, zilipatikana kwa upungufu mkubwa, zikisambazwa kwa usawa usio wa haki, na mataifa yenye kipato cha chini barani Afrika yalizipokea kwa kuchelewa sana.
Mtaalamu wa afya na mwanzilishi wa shirika la Medicines for Africa, Lenias Hwenda, anasema hali hiyo ilikuwa kengele ya tahadhari kwa bara zima. ''COVID-19 ilisababisha mabadiliko makubwa kwa viongozi wa Afrika.
Kabla ya janga hilo, hakukuwa na uelewa wa kutosha kuhusu jinsi gani bara hili lilivyokuwa hatarini kwa kutegemea uagizaji wa asilimia 99 ya chanjo na zaidi ya asilimia 90 ya dawa.''
COVID-19: 'hatua ya mabadiliko' iliyoleta mapinduzi ya dawa Afrika
Mataifa ya Afrika sasa yameweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa ndani wa dawa na chanjo ili kupunguza utegemezi wa muda mrefu. Nchini Senegal, Taasisi ya Pasteur imetengeneza chanjo ya homa ya manjano, huku Ghana, Nigeria, na Ivory Coast zikijenga viwanda vipya. Rwanda, kwa ushirikiano na kampuni ya Ujerumani ya BioNTech, inatarajia kuanza utengenezaji wa majaribio wa chanjo za mRNA mwaka huu, hatua inayotazamwa kama mfano wa mafanikio ya teknolojia ya hali ya juu.
Hata hivyo, utegemezi bado ni mkubwa. Licha ya maendeleo haya, zaidi ya asilimia 90 ya dawa na karibu asilimia 99 ya chanjo bado zinaagizwa kutoka nje, hasa kutoka China na India. Jumuiya za kikanda kama vile yaAfrika Mashariki, EAC na ile ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, zimeanzisha mikakati ya kuimarisha utafiti na uzalishaji wa ndani, kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa ndani kutoka asilimia 1 ya sasa hadi asilimia 60 ifikapo mwaka 2040.
Africa bado inategemea dawa kutoka nje
Hatua kubwa pia imechukuliwa kupitia kuanzishwa kwa African Medicines Agency (AMA) yenye makao yake Kigali, Rwanda, mwaka 2024. Wakala huu unalenga kuoanisha viwango vya udhibiti wa dawa, kushirikisha utaalamu na kuhakikisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa barani humo. Pia, mpango wa African Vaccine Manufacturing Accelerator (AVMA) uliozinduliwa Paris unatarajiwa kuwekeza zaidi ya euro bilioni moja katika kipindi cha miaka kumi, kusaidia kununua zaidi ya dozi milioni 800 za chanjo zinazozalishwa barani.
Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza haja ya uwekezaji wa muda mrefu ili kuhakikisha miradi hii inafanikiwa. Hwenda anashauri kuendeleza miradi iliyoanzishwa sasa kwa uwekezaji endelevu, huku ikiwekeza pia katika vifaa vya uchunguzi na teknolojia za kisasa za afya. Glenda Gray, kutoka Baraza la Utafaiti wa dawa la Afrika Kusini (SAMRC) anasema uwekezaji ni muhimu sana. ''Kwa hivyo tunahitaji kuwekeza zaidi katika ugunduzi, sayansi, kemia ya kikaboni, uhandisi, na kukuza nguvu kazi itakayoweza kukidhi mahitaji ya utengenezaji wa dawa na chanjo barani Afrika.''
Gray anaonya kuwa pamoja na uwezo mkubwa wa nchi kama Afrika Kusini kupitia makampuni kama Biovac na Afrigen, bado kuna upungufu wa utafiti wa awali na teknolojia za kubuni. Anaeleza kuwa hatua za sasa, zikitekelezwa kwa sera thabiti na uwekezaji endelevu, ndizo zitakazoweka msingi imara wa kujenga usalama wa kiafya wa muda mrefu barani Afrika.