Changamoto zinazomkabili Musk na chama chake kipya cha siasa
8 Julai 2025Licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali, Musk anaamini kuwa chama hicho kitawavutia wanachama wa Republican na hata wa Democrats, lakini wachambuzi wanasema kunahitajika mikakati ya muda mrefu ili kuunda chama cha tatu nchini Marekani.
Kuanzisha chama kipya cha siasa nchini Marekani, si jambo rahisi hata kwa mtu tajiri zaidi duniani. Lakini Elon Musk mmiliki wa kampuni ya Tesla na SpaceX amethubutu kuanzisha chama kipya akisema kinalenga kukabiliana na Warepublican waliounga mkono muswada wa sheria uliopendekezwa na rais Trump kuhusu kupunguza ushuru na matumizi ya idara za umma.
Kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii anaoumiliki pia wa X (zamani Twiter), Musk amekinasibu chama chake kama chenye mrengo wa kati kinachojikita zaidi kwenye masuala ya teknolojia, bajeti, nishati, na kikiwa na lengo la kuwavuta upande wake wanachama wa Democrats na Republican ambao hawafurahishwi na sheria hiyo ya Trump ya kupunguza ushuru ambayo inatazamiwa kuongeza kiasi dola trilioni 3.4 katika deni la Marekani.
Mitazamo ya wachambuzi wa siasa za Marekani
Kulingana na wachambuzi wa masuala ya siasa, kusambaratisha ushawishi wa vyama vikuu viwili vya siasa nchini Marekani , kunahitaji nguvu ya ziada na mikakati kabambe inayotakiwa kuendelezwa kwa muda mrefu. Wataalamu hao wanakumbushia kwamba majaribio kadhaa kama hayo yalishindwa huku nyuma na kusisitiza ilivyo vigumu kujipenyeza katika nchi ambayo uchaguzi wake hufanyika jimbo kwa jimbo.
David A. Hopkins, Profesa wa siasa katika Chuo cha Boston ameelezea changamoto lukuki zilizipo kabla ya kufanikisha kuunda chama cha siasa chenye uwezo kamili nchini Marekani, ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu mbalimbali kwa ajili ya chama, kuandaa timu ya watu wa kujitolea kwa ajili ya harakati mbalimbali na zaidi sana kukamilisha vigezo vya kisheria ili kushiriki uchaguzi.
Lakini David Jolly, mbunge wa zamani wa chama cha Republican kutoka Florida na ambaye alikihama chama hicho kutokana na sera za Trump , anasema Musk anaweza kuleta mchango mkubwa wa fedha ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikihitajika ili kutimiza lengo hilo la kuunda chama kipya cha siasa.
Jolly ametolea mfano kwamba ili kukiimarisha chama kipya na kuweza kuwasilisha maombi kwenye tume ya shirikisho ya uchaguzi, kunahitajika kuwepo matawi katika majimbo 50, jambo ambalo linaweza kugharimu hadi dola milioni 100.
Ni vigumu kiasi gani kuunda chama cha siasa Marekani
Mnamo mwaka 2016, Meya wa zamani wa New York na bilionea Michael Bloomberg, alitupilia mbali wazo la kushiriki kinyang´anyiro cha urais kama mgombea huru, akisema kwamba asingelikuwa na "nafasi ya kushinda."
Wataalam wa siasa za Marekani wanakadiria kwamba Musk atahitaji karibu miaka 10 na wastani wa dola bilioni 1 ili kuanzisha chama cha siasa katika ngazi ya shirikisho na chenye uwezo wa kutosha. Wataalamu wengine hata hivyo wanatilia shaka uthabiti wake katika siasa hasa kutokana na matukio ya hivi karibuni baada ya kuenguliwa katika Idara ya Ufanisi wa Serikali jambo linaloashiria kwamba huenda bilionea huyo mwenye asili ya Afrika Kusini hana dhamira ya muda mrefu kwenye masuala ya siasa.
Musk ambaye kulingana na kura ya maoni ya hivi karibuni, anatazamwa vibaya kuliko Trump na Wamarekani hajazungumzia chochote juu ya tathmini hizi za wachambuzi lakini ameonekana kuamini kuhusu kufanikiwa kwa hatua yake hiyo ya kuanzisha chama kipya cha siasa.
(Chanzo: Reuters)