CHAN: Tanzania kuvaana na Morocco robo fainali
18 Agosti 2025Morocco imetwaa ubingwa wa CHAN mara mbili huku Taifa Stars ikitinga hatua hii kwa mara ya kwanza baada ya kushiriki mara tatu.
Mchezo huo utapigwa Agosti 22 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, na utakuwa mchezo wa tano wa CHAN kwa Taifa Stars katika uwanja huo, na hawajapoteza mchezo wowote.
Kocha wa Taifa Stars Hemed Suleiman amesema kuelekea mchezo huo "Nimeangalia makundi yote naamini kwamba kila timu katika kundi lolote ni mzuri na anaweza kuleta ushindani. Sisi tupo tayari kukabiliana na Morocco."
Taifa Stars yasema iko imara kukabiliana na Morocco
Mchezaji wa Taifa Stars, Lusajo Mwaikenda naye kwa upande wake amesema "Tutapambana kwa maana tunajua tunaenda kwenye hatua ya mtoano. Tunafahamu sisi kama wachezaji tunaenda kwenye mchezo mgumu lakini tupo tayari."
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi alisema "Nawapongeza kwa kufuzu hatua ya robo fainali na sasa tujiandae na robo fainali dhidi Morocco lakini pia Nusu fainali. Watanzania Wanajivuania hatua mliyofika kwa maana Timu ya Taifa ni timu ya ushindi."
Mara ya mwisho Timu hizi zilikutana Machi 26, 2025 katika kinyanganyiro cha kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Dunia na Stars ilipoteza kwa mabao 2-0. Morocco na Tanzania zimekutana mara saba katika mashindano yote, na Morocco imeshinda mara sita huku Stars ikishinda mara moja
Wachambuzi: Timu zote zatakiwa kujiandaa vyema
Mchambuzi wa Soka Jastin Mhalinga amesema kuelekea mchezo huo, "Mchezo utakuwa mgumu kwa timu zote mbili. Tanzania imekuwa kwenye kiwango bora kwenye kundi B ikishinda michezo 3 na kutoa sare mechi moja lakini licha ya Morocco kupoteza mchezo dhidi ya Kenya haijawafanya wasifuzu.
Mchambuzi huyo ameongeza "Tanzania inapaswa kuwa makini na washambuliaji wa Morocco ambao wameonekana kuwa na ubora wa kutumia nafasi. Mfano Oussama Lamlioui ambaye mpaka sasa ndio mchezaji nyota wa Morocco akiwa na mabao 3 na mfungaji bora wa michuano ya CHAN 2024 mpaka sasa. Lakini Morroco nao wanapaswa kuwa makini na mshambuliaji wa Tanzania Clement Mzize ambae amekuwa na ubora wa kutumia nafasi."
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Taifa Stars kukipiga dhidi ya Morocco katika michuano ya CHAN 2024. Morocco ambayo imemaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye kundi A, sasa itakwenda Tanzania kukabiliana na Taifa Stars iliyotinga hatua hiyo kabla ya mechi za mwisho za hatua ya makundi baada ya kushinda mechi tatu mfululizo.
Katika hatua ya makundi, Morocco imeshinda mechi tatu na kuchapwa moja dhidi ya Kenya. Imefunga mabao manane sawa na wastani wa kufunga mabao mawili katika kila mechi na kuruhusu mabao matatu.