CHAN: Sudan kukipiga na Madagascar kwa Mkapa
25 Agosti 2025Sudan wameonyesha ustadi katika hatua za mtoano, ikiwemo ni kutinga nusu fainali kwa ushindi wa penalti dhidi ya Algeria.
Wakati Madagascar waliwatoa Kenya Katika Hatua ya Robo Fainali kwa Mikwaju ya Penalti na wanaingia katika Mchezo huo wakiwa na Kumbukumbu ya Mwaka 2023, ambapo waliwafunga Sudan 3–0 kwenye mechi ya kundi katika CHAN.
Katika Mkutano na Waandishi wa Habari Kocha wa Timu ya Taifa ya Sudan amesema amefurahia kufikia hatua ya nusu fainali na wataendelea kupambana.
Kwa upande wa Kocha wa Madagascar Romuald Rakotondrabe amesema kikosi chake kinaendelea kufanya maandalizi kuelekea mechi ya Kesho.
Madagascar atakwaana na Sudan katika uwanja wa Benjamin Mkapa saa 11 Jioni Wakati Morocco atachuana na Senegal.
Kenya yapinga matokeo ya robo fainali
Huku haya yakijiri Gavana wa zamani wa Nairobi, Kenya, Mike Mbuvi Sonko, sasa anataka mchezo wa robo fainali ya Kombe la Mataifa Afrika (CHAN) 2024 kati ya timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, na Madagascar urudiliwe. Sonko ameeleza kuwa kulikuwa na upendeleo na uamuzi usio wa haki kutoka kwa waamuzi katika mchezo huo.
Katika malalamiko aliyowasilisha kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa mujibu wa Kifungu cha 43 cha Katiba ya CAF, Sonko anadai kuwa waamuzi walionyesha upendeleo wazi na kuzuia bila haki magoli mawili yaliyofungwa na Kenya bila kupitia matukio hayo kupitia VAR au kushauriana na makapteni wa timu, makocha, au maafisa wengine.
Kupitia wakili wake Arnold Oginga, Sonko anasema kwamba Kanuni za CAF zinaelezea majukumu ya waamuzi na wafanyakazi wengine walioteuliwa na CAF au FIFA. Anadai waamuzi hao walikuwa na lengo la pamoja na walikusudia kuwanyima Kenya fursa ya haki ya kuendelea hatua ya nusu fainali.
Miongoni mwa hatua anazotaka ni kubatilishwa kwa uamuzi wa kuzuia magoli mawili, kufuta matokeo ya penalti, na kupewa ushindi timu ya Harambee Stars. Kwa mbadala, Sonko anataka CAF iamuru mchezo wa robo fainali urudiliwe.
Safari ya mafanikio ya Kenya katika Kombe la Mataifa Afrika (CHAN) ilimalizika kwa masikitiko Ijumaa usiku baada ya Harambee Stars kuondolewa kwenye robo fainali kwa kupoteza kwa penalti 4-3 dhidi ya Madagascar katika Uwanja wa Michezo wa Kimataifa wa Moi, Kasarani.