Chama cha upinzani Uturuki chaitisha maandamano Istanbul
8 Septemba 2025Matangazo
Chama kikuu cha upinzani nchini Uturuki Republican People's Party, CHP kimewatolea wito Waturuki na wakaazi wa mji mkuu Istanbul wajitokeze kwa maandamano baada ya polisi kuweka vizuizi katika maeneo yanayoyazunguka makao yake makuu mjini humo, katika kile ambacho kiongozi wa chama hicho amekieleza kuwa ni mzingiro.
Chama cha CHP kinaandaa maandamano mengine hivi leo asubuhi. Chama hicho kimelengwa katika wimbi la ukandamizaji wa kisheria ambao umewaangusha mamia ya wanachama wake akiwemo meya wa Istanbul Ekrem Imamoglu, hasimu mkuu wa kisiasa wa rais Recep Tayyip Erdogan, ambaye kukamatwa kwake mwezi Machi kulizua maandamano makubwa kabisa ya barabarani kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha muongo mmoja.