PPRD: Kabila amerejea Kongo kusaka suluhu ya vita
26 Mei 2025Duru mjini Goma zimesema kuwa Joseph Kabila alikuwa na mashauriano na watu wake wa karibu mchana wa Jumatatu mjini huko.
Lakini agenda yake rasmi haijawekwa wazi. Ramazani Shadari, Katibu mkuu wa chama cha PPRD, chama chake Kabila, ameiambia DW kuwa ziara ya Kabilka mjini Goma inalenga kurejesha amani na usalama.
"Kuwasili kwake Goma kunamaanisha kwamba (Joseph Kabila) anatafuta amani kwa Kongo, sababu yeye alikuwa rais na anafahamu vyema changamoto za taifa. Kwetu sisi tunachotaka ni amani irejee nchini Kongo", alisema Shadari.
Duru zimeiambia DW kwamba rais huyo wa zamani wa Kongo aliwasili Goma usiku wa manane kwa njia ya barabara. Na alipokelewa na kiongozi wa kundi la waasi la AFC/M23, Corneille Nangaa. Kabila aliondolewa kinga yake ya kisheria wiki iliopita kufuatia ombi la serikali la kutaka afunguliwe mashtaka ya uhaini.
Serikali ya Kongo imekuwa ikimtuhumu kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaoshikilia miji ya Goma na Bukavu miji mikuu ya majimbo ya Kivu Kasknini na Kivu Kusini.
Je, Kabila amepitwa na wakati ?
Ijumaa iliopita (23.05.2025), Kabila alimkosoa Rais Félix Tshisekedi kwa kile alichokiita uongozi mbaya, akisema kuwa umelitumbukiza taifa katika mgogoro wa "kimuundo" na kuifanya Kongo kuwa kichekesho mbele ya jamii ya kimataifa.
Mjini Kinshasa, hotuba ya Joseph Kabila na ziara yake huko Goma vimechukuliwa kama kitendo cha usalati wa taifa na kwa demokrasia. Akihojiwa na televisheni ya taifa, msemaji wa serikali ya Kongo, Patrick Muyaya amesema kuwa Kabila amepitwa na wakati na alitakiwa kunyamaza.
"Tumeona maoni ya Wakongo baada ya hotuba ya Kabila. Maoni ya Wakongo waliowengi kwenye mitandao ya kijamii ni ishara tosha kuhusu wanachofikiria : kwa hakika, Rais Kabila amepitwa na wakati, ambaye hana jambo jipya la kupendekeza kwa ajili ya mustakbali wa taifa." alisema Muyaya, kabla ya kuongeza :
"Kwa upande wetu, sisi tunajikita katika kutatua matatizo ambayo yeye Kabila hakuweza kuyatatua wakati alipokuwa madarakani."
"Wanachokifanya ni mzaha"
Kuwasili huko kwa Joseph Kabila mjini Goma kunakiweka matatani chama chake cha PPRD ambacho baadhi ya viongozi wake wamekuwa wakihojiwa na mamlaka za Kinshasa huku waziri wa mambo ya ndani akitangaza kusitisha shughuli za chama hicho.
Hata hivyo Ramazani Shadari amesema hawatishiki na hatua hiyo ya serikali.
"Chama ni katika moyo wa mtu na kichwani mwake. Sisi ni wanachama wa PPRD na tutaendelea kuwa wanachama. Wanachokifanya ni mzaha na mchezo mtupu."
Kwenye ujumbe kupitia ukarasa wake wa X, Corneille Nangaa amesema kwa pamoja na Kabila wanadhamiria kukomesha kile alichokiita kuwa ni udikteta na migawanyiko nchini Kongo.