CHADEMA yaenguliwa uchaguzi mkuu ujao
13 Aprili 2025Chadema imemshutumu Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutumia mbinu za ukandamizaji zilizotumiwa na mtangulizi wake, hayati John Pombe Magufuli.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki imeendelea kuwabinya wapinzani wake kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, mwaka huu.
Soma pia: CHADEMA: Vuguvugu letu ni la kutaka mageuzi sio uhaini
Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Tundu Lissu, ambaye alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini mapema wiki hii, hapo awali alieleza kuwa chama hicho cha upinzani hakitoshiriki uchaguzi bila ya kuwepo mageuzi katika mfumo wa uchaguzi.
CHADEMA yasusia kutia saini kanuni za maadili ya uchaguzi
Mnamo siku ya Jumamosi, CHADEMA kupitia Katibu Mkuu wake John Mnyika, alisema hatohudhuria kikao cha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi INEC kwa ajili ya kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi zilizowekwa na serikali.
Uamuzi huo wa kutohudhuria kikao cha INEC ulitokana na kile CHADEMA ilichosema ni "kukosekana kwa majibu kwa njia ya maandishi” kuhusu mapendekezo na madai ya chama hicho ambayo yanatajwa kuwa muhimu kwa ajili ya mageuzi muhimu ya mfumo wa uchaguzi, taarifa ya chama ilisema.
Soma pia: Lissu awakosoa viongozi wa Afrika kwa kujilimbikizia madaraka
Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi INEC Ramadhani Kailima alisema baada ya kikao hicho kuwa, "chama chochote ambacho hakijasaini kanuni za maadili ya uchaguzi hakitaruhusiwa kushiriki katika uchaguzi mkuu au uchaguzi wowote ule kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.”
"Hakutakuwa na nafasi nyingine,” Kailima aliwaambia waandishi wa habari.
Mkurugenzi huyo wa INEC hakuitaja CHADEMA kwa jina, na chama hicho cha upinzani hakijatoa tamko lolote kuhusu uamuzi huo wa INEC.
Tanzania inatarajiwa kufanya uchaguzi wa rais na ubunge mwezi Oktoba.
Chama tawala CCM, chake Rais Samia Suluhu Hassan kilipata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana.
CHADEMA ilidai kuwa uchaguzi huo wa serikali za mitaa uligubikwa na visa vya udanganyifu, na kusema kitawasilisha kesi katika Mahakama kuu kikitaka mageuzi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Lissu mwaka jana alionya kuwa CHADEMA kingezuia uchaguzi kwa "njia za mgongano” hadi pale mfumo wa uchaguzi utakapofanyiwa marekebisho.
Soma pia: Je, kuna mpasuko ndani ya Chadema?
Matakwa ya upinzani yamekuwa yakipuuzwa kwa muda mrefu na chama tawala.
Awali, Rais Samia alipongezwa kwa kulegeza masharti yaliyowekwa na mtangulizi wake hayati John Magufuli dhidi ya upinzani na vyombo vya habari katika taifa hilo lenye idadi ya watu wapatao milioni 67.
Hata hivyo, makundi ya kutetea haki za binadamu na serikali za mataifa ya Magharibi zimeikosoa serikali ya Samia kwa kile walichokieleza ni kurejea kwa ukandamizaji, ikiwa ni pamoja na kamatakamata ya wanasiasa wa CHADEMA pamoja na visa vya utekaji na mauaji ya wanasiasa wa upinzani nchini humo.